Ufaransa yawasaka washambuliaji wa mkasa wa ugaidi | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ufaransa yawasaka washambuliaji wa mkasa wa ugaidi

Polisi wa Ufaransa wameanzisha msako mkali kote nchini humo kuwatafuta watu waliohusika katika mashambulizi ya Juma lililopita mjini Paris lililosababisha watu 129 kuuwawa

Serikali za Ufaransa na Ubelgiji zimeimarisha msako huo wa kuwatafuta washambuliaji pamoja na washirika wao walioshiriki mashambulizi ya ijumaa katika mabaa, migahawa pamoja na kiwanja cha mpira, yaliosababisha mauaji ya watu 129, wengi wao wakiwa vijana.

Polisi kwa sasa wanamtafuta Salah Abdeslam, aliye na miaka 26 mmoja wa ndgugu watatu wa kiume wanaoaminika kushiriki katika shambulizi hilo, huku wachunguzi wakiamini mpiganaji wa jihadi raia wa Ubelgiji Abdelhamid Abaaoud, ambapo makao yake ni Syria ndiye aliyepanga shambulizi hilo.

Polisi wa Ufaransa akimsaidia mtu aliyejeruhiwa baada ya mashambulizi ya kigaidi

Polisi wa Ufaransa akimsaidia mtu aliyejeruhiwa baada ya mashambulizi ya kigaidi

"Hatujui iwapo kuna washirika Ubelgiji na Ufaransa, Bado hatujajua idadi ya watu waliohusika katika shambulizi hilo," alisema Waziri Mkuu Manuel Valls alipozungumza na redio moja ya Ufaransa.

Aidha polisi nchini humo waliendesha misako 128 kote nchini iliyolenga mitandao ya wanamgambo walio na itikadi kali, siku moja baada ya operesheni kama hiyo kufanikiwa kupata silaha chungu nzima Kusini Mashariki mwa mji wa Lyon, hii ikiwa ni kwa mujibu wa Waziri wa ndani wa Ufaransa Bernard Cazeneuve. Waziri Cazeneuve amesema watu 100 wamewekwa katika kifungo cha nyumbani huku wengine 23 wakikamatwa.

Kerry asema ushirikiano zaidi unahitajika kupambana na IS

Kwengineko Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amekutana na rais Francois Hollande kujadili mipango ya kujibu mashambulizi ya Ijumaa na kutafuta njia ya kumaliza mgogoro wa Syria. Baada ya mazungumzo hayo Waziri Kerry alisema pamoja na mengine walizungumzia namna ya kurefusha ushirikiano dhidi ya kundi la IS.

Huku hayo yakiarifiwa Wizara ya ulinzi ya Ufaransa imesema ndege zake za kivita zimeshambulia ngome za wanamgambo wa dola la kiislamu nchini Syria na kuharibu kituo cha mawasiliano na kituo cha mafunzo mjini Raqa.

Waziri wa nje wa Marekani John Kerry

Waziri wa nje wa Marekani John Kerry

Rais wa Ufaransa Francois Hollande ameapa kulishambulia kundi hilo bila huruma baada ya mashambulizi ya juma lililopita yaliyotokea chini ya mwaka mmoja baada ya mashambulizi ya siku tatu yaliosababisha mauaji ya watu 17 ikiwemo shambulizi katika ofisi ya jarida la vibonzo la Charlie Hebdo na soko la wayahudi.

"Mashambulizi ya Ijumaa yaliamuliwa Syria, yakatayarishwa na kupangwa Ubelgiji na kutekelezwa katika taifa letu," alisema rais Hollande alipokuwa anayahutubia mabaraza mawili ya bunge. "Umuhimu wa kulitokomeza kundi hili la IS unajumuisha jamii nzima ya Kimataifa aliwaambia wabunge walioanza mara moja kuimba wimbo wa taifa la Ufaransa, baada ya hotuba ya rais.

Mwandishi: Amina AbubakarAFP/dpa/AP

Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com