1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha FN cha Ufaransa chamtimua muasisi

21 Agosti 2015

Chama cha mrengo mkali wa kulia nchini Ufaransa cha National Front, FN kimemfukuzwa muasisi wake Jean-Marie Le Pen, kutokana na kauli zake za kibaguzi ambazo zimekiweka matatani chama hicho kwa miezi kadhaa.

https://p.dw.com/p/1GJZh
Jean-Marie Le Pen, muasisi wa chama cha FN
Jean-Marie Le Pen, muasisi wa chama cha FNPicha: Getty Images/AFP/M. Bureau

Uamuzi wa kumtimua Le Pen ulifikiwa na uongozi wa chama hicho, baada ya mjadala mrefu na mkongwe huyo karibu na mji mkuu, Paris. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, viongozi wakuu wa chama hicho cha Front Nationale, au FN kwa ufupi, akiwemo mwenyekiti wa chama hicho wa sasa, Marine Le Pen ambaye ni binti yake Jean Marie Le Pen, wamejitenga na mwasisi huyo wa chama chao ambaye ana umri wa miaka 87.

Hatua yao hiyo ilifuatia kauli yake iliyobeza mauaji ya kimbari dhidi ya wayahudi, Holocaust, ambamo alidai kuwa Vyumba vya mateso vilivyotumiwa na utawala wa wanazi kuwauwa wayahudi, havikuwa chochote zaidi ya ''maelezo ya kihistoria''.

Akerwa na uamuzi wa kumtimua

Kabla ya kufukuzwa katika chama hicho jana, Le Pen alijieleza kwa muda mrefu mbele ya kamati kuu ya chama katika mji wa Nanterre ulio karibu na Paris. Baada ya maelezo hayo wajumbe wengi walipiga kura kuunga mkono hatua ya kumfukuza.

Marine Le Pen aliyechukuwa uongozi wa FN kutoka kwa baba yake
Marine Le Pen aliyechukuwa uongozi wa FN kutoka kwa baba yakePicha: Getty Images/AFP/D. Charlet

Akizungumza baada ya hatua hiyo dhidi yake, Jean Marie Le Pen alisema amechukizwa na kitendo hicho, ambacho alikifananisha na shambulio la kuvizia.

''Kama mnavyoona, kichwa changu bado kiko juu ya mabega, kwa hiyo kila kitu ni salama. Nilitumai kutowachukulia walokuwa wakinihoji kama majaji, kwa sababu sina imani na uwezo wao kufanya hivyo'', amesema Le Pen, na kuongeza kuwa yeye kama mwanaharakati, ameeleza wazi maoni yake kwamba kikao hicho kilikuwa chenye utata.

Baadhi ya wafuasi wa mwasisi huyo wa chama cha FN wamekasirishwa na kufukzwa kwake, akiwemo mbunge wa chama hicho katika bunge la Umoja wa Ulaya Bruno Gollnisch ambaye amesema kimaadili, uamuzi huo ulikuwa ni kushtusha.

Mpasuko wa kifamilia

Binti yake Jean Marie Le Pen, Marine Le Pen alirithi uongozi wa chama hicho mwaka 2011, lakini kauli za kibaguzi za baba yake zimekuwa kizingiti kikubwa kwa ndoto zake kuelekea Ikulu ya Ufaransa.

Kauli za kibaguzi za Jean-Marie Le Pen zimetatiza juhudi za bintie kuelekea Ikulu
Kauli za kibaguzi za Jean-Marie Le Pen zimetatiza juhudi za bintie kuelekea IkuluPicha: Reuters/P. Wojazer

Uhasama wa wazi ulidhihirika kati ya Jean Marie le Pen na binti yake mwezi Aprili mwaka jana, pale mkongwe huyo aliposhikilia kauli zake za awali zinazoyakanusha mauaji ya wayahudi. Hata hivyo binti yake hakushiriki katika kikao cha jana.

Tayari mahakama nchini Ufaransa imetengua mara mbili uamuzi wa chama cha FN kutaka kumtenga mwasisi wake huyo, ambaye anaendelea kuwa rais wa heshima wa chama hicho, baada ya kushinda rufaa za maamuzi ya kumfukuza.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae/rtre

Mhariri:Ssessanga