1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi mkuu wafanyika Zimbabwe

31 Julai 2013

Raia wa Zimbabwe siku ya Jumatano wanafanya uchaguzi mkuu. Upinzani mkali upo kati ya Robert Mugabe na waziri mkuu Morgan Tsvangirai wanaogombea nafasi ya urais. Hatma ya Mugabe itaamuliwa katika vituo vya kupigia kura.

https://p.dw.com/p/19Hdt
Mpiga kura Zimbabwe
Mpiga kura ZimbabwePicha: picture-alliance/dpa

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa moja asubuhi kwa saa za Zimbabwe. Watu wengi waliwahi mapema na kupanga foleni mbele ya vituo wakiwa wamevaa sweta na makoti mazito kwa ajili ya kujikingia na baridi. Masaa manne baada ya vituo kufunguliwa, watu wengi waliofika mapema sana bado walikuwa hawajapata nafasi ya kuingia katika vituo vya kupgia kura.

"Tunasubiri hapa kuanzia saa moja na nusu asubuhi mpaka sasa hivi. Mambo yanakwenda taratibu sana. Sijui ni nini kinachoendelea huko ndani. Tungekuwa na vituo vingi zaidi labda mambo yangekwenda haraka zaidi. Tumechoka kusimama katika foleni," alisema mpiga kura huyo.

Shutuma za wizi wa kura

Takriban raia milioni 6.4 wana haki ya kupiga kura leo. Tume ya uchaguzi ya Zimbabwe imekiri kwamba pamekuwa na hitilafu katika maandalizi ya uchaguzi wa leo lakini imesema vituo vyote 9,000 sasa viko tayari kutumiwa na wapiga kura watakaofika.

Foleni ya wapiga kura mbele ya kituo
Foleni ya wapiga kura mbele ya kituoPicha: Alexander Joe/AFP/Getty Images

Kipindi cha kampeni za uchaguzi kiligubikwa na shutuma za wizi wa kura kwa upande wa chama tawala. Utafiti uliofanywa Zimbabwe na shirika moja lisilo la kiserikali mwezi Juni ulionyesha kwamba zaidi ya majina milioni moja yaliyosajiliwa katika madaftari ya wapiga kura yalikuwa ya watu waliokufa. Pamoja na hayo, zaidi ya watu laki moja wana umri wa zaidi ya miaka 100, jambo lililowafanya watafiti washuku uhalisia wa majina hayo.

Mugabe na Tsvangirai si wagombea pekee. Welshman Ncube ni mgombea wa urais wa chama cha MDCN kilichojitenga na chama cha MDC cha waziri mkuu Tsvangirai.

"Tunachotarajia ni uchaguzi wa haki. Tunachotarajia ni matokeo halali," alisema Nnube.

Tsvangirai apewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda

Zimbabwe bado inakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi. Katika kampeni yake, Mugabe aliahidi kugawa mali ya nchi ili iweze kufikia wananchi maskini.

Robert Mugabe na mpinzani wake Morgan Tsvangirai
Robert Mugabe na mpinzani wake Morgan TsvangiraiPicha: AP

Kwa upande wake, Tsvangirai anataka kuwahimiza wawekezaji kutoka nje kufungua viwanda na biashara Zimbabwe. Ameahidi pia kutengeneza nafasi mpya za kazi milioni moja na kuboresha huduma kwa umma.

Maoni ya wapiga kura yanaonyesha kwamba Tsvangirai anapewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda. Asilimia 61 ya waliohojiwa walisema kwamba wanakipendelea chama cha MDC cha Tsvangirai huku asilimia 27 tu wakikiiunga mkono chama cha ZANU-PF cha Robert Mugabe.

Vituo vya kupigia kura vitafungwa saa moja jioni kwa saa za Zimbabwe. Matokeo kamili yanatarajiwa kutolewa katika kipindi cha siku tano zijazo.

Mwandishi:Elizabeth Shoo/afp/ap

Mhariri:Yusuf Saumu