1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi EU: Ni mchanganyiko wa vilio na furaha

Iddi Ssessanga
27 Mei 2019

Uchaguzi wenye ushindani mkali katika miongo kadhaa umekamilika Ulaya kwa vyama vinavyopinga wageni na watetezi wa mazingira wakizidi kupata umaarufu. Kukubalika kwa vyama hivyo kumekuja kwa gharama ya vyama vikongwe.

https://p.dw.com/p/3J9L2
Belgien Margrethe Vestager in Brüssel
Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Seco

Uchaguzi huo uliodumu kwa siku nne katika mataifa 28 ya kanda ya Umoja wa Ulaya ulitazamiwa kuwa kipimajoto cha wimbi la ushawishi wa serikali za kizalendo, siasa kali na mavuguvugu ya itikadi kali za mrengo wa kulia ambalo limelikumba bara la Ulaya katika miaka ya karibuni na kuisukuma Uingereza kuondoa katika Umoja wa Ulaya.

Wakati vyama vinavyoupendelea Umoja wa Ulaya vinaelekea kushinda theluthi mbili ya viti vya bunge hilo, vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia na watetezi wa mazingira (Kijani) vilionekana kupata mafanikio makubwa, kwa mujibu wa makadirio yaliotolewa na bunge la Ulaya.

Matine Le Pen amfedhehesha rais Emmanuel Macron

Makadirio nchini Ufaransa yalikuwa yakionyesha chama cha mrengo mkali wa kulia chake Marine Le Pen - kinachopinga uhamiaji cha National Rally kimeibuka na ushindi na kumfedhehesha rasi Emmanuel Macron, ambaye aliufanya ushirikiano wa Umoja wa Ulaya ajenga kuu ya urais wake.

Europawahlen Frankreich Marine Le Pen Rassemblement National
Kiongozi wa chama cha National Rally Marine Le Pen, ambacho kimeshinda Ufanransa.Picha: Reuters/C. Platiau

Le Pen alisema matokeo hayo "yanathibitisha mgawanyo wa kimataifa ya siasa za kizalendo nchini Ufaransa na kwingineko.

Makadirio ya matokeo nchini Ujerumani yalionyesha chama cha kansela Angela Merkel na mshirika wake serikali - chama cha siasa za wastani za rmengo wa kushoto pia vimepoteza viti vingi.

Huku shinikizo likizidi kuwa kubwa, muitiko wa wapigakura - ukitoa Uingereza, ambayo inaondoka kwenye kanda hiyo - uliwekwa kwa asilimia 51, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi katika kipindi cha miaka 20.

Matteo Salvin aongoza Italia

Chama cha Matteo Salvin cha League kimeshinda kura nyingi zaidi katika uchaguzi wa bunge la Ulaya nchini Italia kwa kupata kati ya asilimia 27-31 kwa mujibu wa matokeo ya awali.

Matokeo hayo yanaimarisha udhibiti wa waziri wa mambo ya ndani Salvin kwenye serikali, baada ya mshirika wake - Vuguvugu la Five Star (M5S) kupitwa na chama kinachofufuka upya cha Democratic (PD), kilichishika nafasi ya pili kwa kupata kati ya asilimia 21-25.

Chama cha M5S chake Luigi Di Maio kimepata asilimia kati ya 18.5 - 22.5 ya kura, huku chama cha Forza Italia, cha tajiri na waziri mkuu wa zamani Silivio Berlusconi kikipata asilimia 12 ya kura.

Uingereza yagawika kuhusu Brexit

Chama cha Brexit, chake Nigel Farage kilikuwa njiani kupata ushindi katika uchaguzi wa bunge la Ulaya huku vyama vikuu vya Conservative na Labour vikipoteza uungwaji mkono nchini kote, kulingana na matokeo ya awali.

Kushindwa kwa waziri mkuu Theresa may kuitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya kunaelezwa kuwa sababu iliyowakasriisha wapigakura na kuamua kukiadhibu chama chake pamoja na kile cha Labour.

Großbritannien Nigel Farage in Southampton
Kicheko hatari: Nigel Farage na chama chake kipya cha Brexit ndiyo wameibuka washindi nchini Uingereza, na sasa anataka usemi zaidi katika mchakato wa Brexit.Picha: AFP/T. Akmen

Uingereza ilipaswa kuondoka rasmi kwenye Umoja wa Ulaya Machi 29 lakini bado imebakia kuwa mwanachama wa umoja huo na wanasiasa wake wanaendelea kubishana juu ya vipi, lini au hata iwapo nchi hiyo itaondoka katika klabu hiyo iliyojiunga nayo mwaka 1973.

Nchini England na Wales, wapigakura walikiacha kwa hasira chama cha May na cha Labour chake Jeremy Corbyn, ambacho kilitaka mchakato laini wa Brexit. Chama cha Conservative kilikuwa njiani kupata matokeo yake mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika uchaguzi wa kitaifa.

Makadirio ya shirika la utangazaji la BBC yamekipa chama cha Conservative karibu asilimia 10 hadi 12,  kikishuka kutoka asilimia 23 ya mwaka 2014. Labour ilishika nafasi ya tatu jimboni Wales. Chama cha Liberal Democrats kilishinda hata katika jimbo la nyumbani la Corbyn, Islington.

Wasoshalisti wa Uhispania walenga kupambana dhidi ya ubanaji matumizi

Waziri Mkuu msimamizi nchini Uhispania Pedro Sanchez anasema chama chake cha Kisoshalisti kitashinikiza ajenda ya ustawi wa kijamii na kupinga mkakati wa kubana matumizi baada ya kushinda uchaguzi wa bunge la Ulaya.

Baada ya kuhesabiwa asilimia 98 ya kura Jumapili jioni, Wasoshalisti walishinda viti 20 kati ya 54 ilivyotengewa Uhispania katika bunge la Ulaya. Sanchez anasema Uhispania itakuwa ujumbe wa juu wa Wasoshalisti kwenye jukwaa la Ulaya.

Spanien - Pedro Sanchez gibt seine Stimme zur Europawahl ab
Kaimu waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez akipiga kura yake nje ya mji wa Madrid Jumapili, Mei 26, 2019. Chama chake cha kisoshalisti kimeibuka na viti vingi zaidi.Picha: Reuters/S. Vera

Sanchez sasa anaweza kujikita katika kujaribu kuunda serikali mpya kufuatia ushindi wa chama chake cha kisoshalisti katika uchaguzi wa taifa wa Aprili 28. Mwitikio nchini Uhispania kwa uchaguzi wa bunge jipya ulikuwa asilimia 64.3, kutoka asilimia 45.8 mwaka 2014.

Hakuna ushirikiano na vyama vya kizalendo

Viongozi wa kambi mbili za vyama vikuu katika bunge la Ulaya wameondoa uwezekano wa kushirikiana na vyama vya kizalendo vilivyopata mafanikio katika uchaguzi wa mwaka huu, na wametoa wito wa kuunda ushirikiano miongoni mwa vyama vinavyopendelea Umoja wa Ulaya.

Manfred Weber, kiongozi wa kambi ya mrengo wa wastani wa kulia EPP, alisema Jumapili usiku kuwa "kuanzia sasa, wale wanaotaka kuacha Umoja wa Ulaya ulioimara wanapaswa kuungana."

Weber anasema kambia yake haitoshirikiana na chama chochote kisichoamini katika mustakabali wa Umoja wa Ulaya."

Frans Timmermans, kiongozi wa wasoshalisti na wademokrat ambaye ndiye mpinzani mkuu wa Weber kwa nafasi ya rais wa halmashauri kuu ya Ulaya, anasema anataka kushirikiana na vyama vya mwendelezo "kujaribu kujenga program inayoshughulikia ndoto hizo, na pia wakati mwingine hofu za Waulaya wenzetu.

Griechenland Athen - Manfred Weber der CSU und EPP-Kandidat für die Europawahl bei Rede
Manfred Weber, kiongozi wa kundi la EPP na mgombea wa nafasi ya rais wa Halmashaurki Kuu ya Umoja wa Ulaya.Picha: Getty Images/AFP/L. Gouliamaki

Mgawanyo wa viti mpaka sasa

Kambi ya EPP inatazamiwa kushinda viti 180 na ile ya S&D itakuwa na viti 152 katika bunge lenye jumla ya viti 751 kulingana na makadirio ya Umoja wa Ulaya.

Wakati huo huo kambi ya Kiliberali ya ALDE imepata mafanikio makubwa, na kuongeza viti vyake hadi 105, ikiwemo orodha ya Renaissance ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Kambi ya vyama vya Kijani iinashika nafasi ya nne ikiwa na viti 67, baada ya kupata mafanikio katika mataifa kadhaa. Nchini Ujerumani, waliwapiku chama cha Social Democratic SPD katika nafasi ya pili kwa kupata karibu asilimia 21.

Matokeo ya makundi matatu makuu ya vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia katika bunge linalomaliza muda wake yalikuwa chini kuliko baadhi walivyotarajia. Wanaweza kuchukuwa jumla ya viti 172 au karibu asilimia 23 ya viti vya bunge jipya.

Wakati takwimu zinaweza kubadilika wakati matokeo zaidi yakizidi kutolewa na kambi zikijipanga upya, baadhi ya makadirio yalikuwa yameviweka kwa jumla ya asilimia 30 au zaidi.

Uchaguzi ulidumu kwa siku nne na ulikuwa wazi kwa wapigakura zaidi ya milioni 400 wenye vigezo, katika kile kinachoelezwa kuwa uchaguzi mkubwa zaidi unaohusisha mataifa mengi.

Umekuja wakati ambapo Umoja wa Ulaya unajaribu kujipanga upya kuhusiana na mpango wa Uingereza kuondoka, na kukiw ana vitisho kutoka ndani na nje ya kanda hiyo.

Vyanzo: Mashirika