UAE yatangaza kujiondoa Muungano wa OPEC
29 Aprili 2026
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imetangaza kuwa itajiondoa katika Muungano wa Mataifa yanayozalisha mafuta kwa wingi, OPEC kuanzia Mei 1, 2026, hatua inayotarajiwa kuathiri kwa kiasi kikubwa soko la mafuta duniani.
Tangazo hilo linaiondoa moja ya wazalishaji wakubwa wa mafuta katika kundi hilo, ambalo kwa muda mrefu limekuwa na ushawishi mkubwa katika kudhibiti uzalishaji na bei za mafuta.
Akizungumza Jumanne, Waziri wa Nishati na Miundombinu wa UAE, Suhail Al Mazrouei, alisema uamuzi huo unaendana na mageuzi ya sera ya nishati na mwelekeo wa muda mrefu wa kiuchumi wa nchi hiyo.
Alieleza kuwa hatua hiyo pia inalenga kuwezesha UAE kushirikiana kwa urahisi zaidi na wawekezaji na washirika wa kimataifa katika sekta ya mafuta, gesi na kemikali za petroli.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa uamuzi huo hauchochewi na mvutano wowote na Saudi Arabia, ambayo inaongoza OPEC.
Athari kwa soko la mafuta
UAE imesema imechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya OPEC, lakini sasa inalenga kuipa kipaumbele maslahi yake ya kitaifa katika sekta ya nishati inayobadilika haraka.
Tangazo hilo pia linajumuisha kujiondoa katika muungano mpana wa OPEC+, unaojumuisha mataifa kama Urusi.
Hatua hiyo inatazamwa kama pigo kwa ushawishi wa OPEC na OPEC+, huku wachambuzi wakitarajia kupungua kwa uwezo wa kundi hilo kudhibiti bei za mafuta kimataifa.
Ingawa uamuzi huo hauhusiani moja kwa moja na hali ya Mlango wa Hormuz, unaweza kuathiri bei ya mafuta ikiwa UAE itaongeza uzalishaji wake.
Siku ya Jumanne, bei ya pipa moja la mafuta ghafi ilikuwa juu ya dola 111, ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na viwango vya kabla ya vita.
Nafasi ya UAE katika OPEC
UAE ilijiunga na OPEC mwaka 1967, na imekuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta ndani ya kundi hilo.
Takwimu zinaonyesha kuwa Februari mwaka huu, UAE ilikuwa ya tatu kwa uzalishaji miongoni mwa wanachama wa OPEC, nyuma ya Saudi Arabia na Iraq.
Kwa ujumla, nchi wanachama wa OPEC huchangia takribani asilimia 36ya uzalishaji wa mafuta duniani na kudhibiti karibu asilimia 80 ya akiba ya mafuta iliyothibitishwa.
Kwa sasa, uamuzi wa UAE unafungua ukurasa mpya katika siasa za nishati duniani, huku athari zake zikitarajiwa kujitokeza katika miezi ijayo.