1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tunisia yakabiliwa na mgomo wa kitaifa

8 Februari 2013

Tunisia inakabiliwa na mgomo wa kitaifa leo (08.02.2013), wakati maelfu ya waandamanaji watakapoingia mitaani, kufuatia mauaji ya kiongozi wa mrengo wa kushoto wa upinzani, yaliyosababisha vurugu.

https://p.dw.com/p/17acQ
Watunisia wakiandamana kufuatia mauaji ya Chokri Belaid
Watunisia wakiandamana kufuatia mauaji ya Chokri BelaidPicha: AFP/Getty Images

Chama Kikuu cha wafanyakazi nchini humo cha UGTT kiliitisha mgomo huo utakaokwenda sambamba na msiba wa Chokri Belaid, wakili na mkosoaji mkubwa wa chama tawala cha Ennahda, ambaye alipigwa risasi nje ya makaazi yake.

Waziri Mkuu wa Tunisia, Hamadi Jebali.
Waziri Mkuu wa Tunisia, Hamadi Jebali.Picha: picture alliance/ZUMA Press

Wito wa mgomo uliyotolewa na UGTT ambacho ndiyo chama cha wafanyakazi chenye nguvu zaidi nchini Tunisia, unakuja baada ya mauaji ya Belaid kusababisha maandamano mjini Tunis, na katika mkoa wa kati uliyo na shughuli nyingi za uchimbaji wa Gafsa, huku nchi hiyo ikizidi kujichimbia katika mgogoro wa kisiasa.

Ennahda yapinga uamuzi wa waziri mkuu

Belaid atazikwa baada ya swala ya Ijumaa katika taifa hilo la Kiislamu, ambako utamaduni wa muda mrefu wa siasa zisizo egemea dini, umekabiliwa na kuibuka kwa moja ya vyama vyenye nguvu zaidi vya Kiislamu katika kanda. Baada ya kuripuka kwa hasira za wananchi dhidi ya mauaji ya Belaid, waziri Mkuu Hamad Jebali anayetokea chama cha Ennahda, alisema katika hotuba iliyotangazwa moja kwa moja kupitia luninga siku ya Jumatano, kuwa angeunda serikali mpya inayoongozwa na wataalamu wasiyoegemea upande wowote wa kisiasa.

Lakini kiongozi wa wabunge kutoka chama cha Ennahda, Sahbi Atig alisema jana alhamisi kuwa kundi lake la wabunge limekataa mipango hiyo, na kuongeza kuwa waziri mkuu hana mamlaka ya kuchukua maamuzi pekee yake, na kwamba Tunisia bado inahitaji serikali imara ya kisiasa. Mabadiliko yoyote katika serikali laazima yaidhinishwe na bunge.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Tunisia Mohamed Taunsi, anasema uamuzi uliyotangazwa na Waziri mkuu ni wa hatari kwa demokrasia nchini humo: "Kwangu mimi huo ni umauzi uliyochukuliwa chini ya shinikizo kubwa baada ya tukio la mauaji. Sidhani kama uamuzi wa haraka kama huo ni sahihi. Nadhani serikali halali ikianguka, serikali nyingine hazitaweza.Hiyo ndiyo hofu ya Tunisia. Kilicholetwa kupitia masanduku ya kura laazimakishindwa kupitia masanduku ya kura."

Waandamanaji wakilizingira gali lililobeba mwili wa Chokri Belaid, ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha Patritotic Front.
Waandamanaji wakilizingira gali lililobeba mwili wa Chokri Belaid, ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha Patritotic Front.Picha: picture-alliance/dpa

Viongozi watakiwa kukaa pamoja kutafuta suluhu

Marekani imetoa wito kwa viongozi wa Tunisia kukaa pamoja na kutatua matatizo yanayoikabili nchi hiyo, na kutoa wito wa kuwepo na utulivu. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Victoria Nuland alisema vurugu hazina nafasi katika demokrasia ya Tunisia, na kwamba vurugu haziwezi kutatua changamoto zinazowakabili Watunisia, bali zitachochea tu vurugu nyingine.

Katika mji mkuu Tunis jana Alhamisi, Polisi ilitumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji waliyoingia mitaani licha ya ulinzi mkali katika mtaa wa Habib Bourguiba, ambao ndiyo kitovu cha mapinduzi ya mwaka 2011 yalimuondoa rais Zine El Abidine Ben Ali. Katika mji wa Gafsa, waandamanaji walirushwa mabomu ya petroli kwa polisi, ambayo ilijibu kwa kutumia gesi ya kutoa machozi.

Vyama vinne vya upinzani kikiwemo cha Belaid cha Popular Front vimesema vitajiondoa katika bunge lililochaguliwa Oktoba 2011, lakini ambalo limeshindwa kuunda katiba mpya.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Daniel Gakuba