1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kuwakutanisha Kagame na Tshisekedi kusaini makubaliano

4 Desemba 2025

Rais wa Marekani Donald Trump Alhamisi atakutana na viongozi wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa kile anachojigamba kuwa ni hatua yake ya hivi karibuni ya kusitisha vita, licha ya mapigano yanayoendelea.

https://p.dw.com/p/54k1U
Rais wa Rwanda Paule Kagame | Rais wa Kongo Felix Tshisekedi
Makubaliano ya amani kati ya Rwanda na Kongo yanasainiwa huku mapigano yakiendelea mashariki mwa Kongo Picha: Virginia Mayo/AP/picture alliance

Trump ana matumaini kuwa makubaliano kati ya chi hizo mbili yatafungua njia kwa Marekani kupata udhibiti wa madini muhimu mashariki mwa Kongo, eneo ambalo linakumbwa na vita.

Rais wa Rwanda Paul Kagame, atakutana na Rais wa Kongo, Felix Tshisekedi, ambapo Ikulu ya Marekani, White House imesema watasaini makubaliano ya amani.

Hata hivyo, siku moja kabla ya kusainiwa kwa makubaliano hayo mapigano makali yamezuka mashariki mwa Kongo kati ya kundi la waasi wa M23 na jeshi la Kongo.

Tshisekedi alaani mapigano ya M23

Akizungumzia mashambulizi hayo, Rais Tshisekedi amesema kuibuka tena kwa M23 linaloungwa mkono na Rwanda, kumesababisha mgogoro wa kibinadamu ambao haujawahi kutokea, na kwamba takribani watu milioni 7 ni wakimbizi wa ndani. Amesema uchokozi huo ni ukiukaji mkubwa wa uhuru wa Kongo.

''Tunaitolea wito jumuia ya kimataifa kulaani vikali vitendo hivi na kuweka vikwazo vinavyoilenga Rwanda kwa kuvuruga amani, na tunataka wanajeshi wa Rwanda waondolewe mara moja na bila masharti kutoka kwenye eneo letu,'' alifafanua Tshisekedi.

Makubaliano hayo yatasainiwa ikiwa ni zaidi ya miezi mitano baada ya mawaziri wa mambo ya nje wa Rwanda na Kongo kukutana na Rais Trump na kutangaza makubaliano mengine ya kuumaliza mzozo huo.