Trump ataka bunge kufutilia mbali bima ya afya ya Obama | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.03.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Trump ataka bunge kufutilia mbali bima ya afya ya Obama

Rais Donald Trump asema amehitimisha majadiliano kuhusu sheria ya kuuondoa mpango wa bima ya afya ya Rais wa zamani Barack Obama maarufu Obamacare na kuwataka wabunge kuunga mkono mpango wake katika kura itakayopigwa leo

Tamko hilo la Trump linakuja baada ya Wabunge wa chama cha Republican kutangaza kuwa watachelewesha kura kuhusu mpango wa kuifumua sheria ya huduma ya afya ya Rais wa zamani Barack Obama maarufu kama Obamacare, mpango ambao utapunguza jukumu la serikali katika kuwasaidia watu kumudu bima na huenda ukawaacha Wamarekani wengi bila ya bima ya afya.

Je wabunge wataifutilia mbali Obamacare?

Wabunge wa Republican walipaswa kupigia kura mswada mpya wa afya jana Alhamisi lakini badala yake wakatangaza kuwepo mkutano miongoni mwa wanachama wa chama hicho. Tangazo hilo linaonekana kuwa pigo kwa Rais Donald Trump ambaye alishinda kutwa nzima jana akifanya mikutano ya kujaribu kupata uungwaji mkono kutoka kwa wanachama wa chama chake cha Republican.

USA Donald Trump vor dem US-Kongress in Washington (Getty Images/W. McNamee)

Rais Donald Trump akizungumza na baadhi ya wabunge

Viongozi wa bunge walilalazimika kuahirisha kura hiyo kutokana na baadhi ya Warepublican wenye misimamo mikali kukataa kuidhinisha muswada wa kuwepo bima mpya bila ya mswada huo kufanyiwa mabadiliko muhimu na hivyo kuwa mtihani wa kwanza bungeni kwa rais mpya wa Marekani wa iwapo atawashawishi wabunge wa chama chake walio wengi bungeni kumuunga mkono kuhusu suala hilo la bima ya afya kwa Marekani au la.

Mkurugenzi wa bajeti katika Ikulu ya rais Mick Mulvaney amewaambia wabunge kuwa ametumwa na Rais Trump kuwaeleza kuwa wafanye kila wawezalo kuhakikisha kuwa ifikapo Ijumaa, wawe wamefikia uamuzi kuhusu iwapo huduma ya afya ya Obamacare inaondolewa au la na kama haitakuwa imeamuliwa ifikapo leo basi utawala huo utasonga mbele na mambo mengine.

Mkakati huo wa Trump wa kutoa muda wa mwisho kwa wabunge wa chama chake kufikia maamuzi kunaonekana kulenga kuwashinikiza Warepublican walioasi kusalimu amri na kuunga mkono ajenda zake.

Mamilioni kuathirika iwapo Obamacare itasitishwa

Spika wa bunge Paul Ryan ambaye amekuwa akiunga mkono muswada wa bima mpya ijulikanayo American Health care amewaambia wanahabari kuwa wamekuwa wakiwaahidi Wamarekani kuwa wataifuta bima ya Obamacare kwa sababu inaporomoka na kutoa huduma zisizostahili kwa familia na hivyo watasonga mbele kuhakikisha hilo linafanikiwa.

Washington Supreme Court Entscheid über Obamacare PK Obama (Reuters/G. Cameron)

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama

Bunge linatarajiwa kukutana kwa ajili ya kura hiyo leo mchana saa za Washington. Wengi wa warepublican wanaopinga mpango wa Trump wanasema mpango huo bado ni wa gharama ya juu kwa serikali.

Wanataka kipengele cha kutolewa kwa huduma za kimsingi za afya kama afya ya uzazi, huduma za dharura na huduma za kuzuia magonjwa kama chanjo na uchunguzi wa matibabu ambazo ziko katika Obamacare inayoshurutisha kampuni za bima kusimamia kuondolewa wakihoji inafanya gharama ya  bima ya afya kuwa juu.

Mpango huo wa Warepublican utawaacha Wamarekani milioni 14 bila ya bima ya afya kuanzia mwaka ujao. Wademocrat wamejiandaa kupiga kura kwa kauli moja kwa hivyo viongozi wa Republican wanahitaji kupunguza idadi ya wanaoupinga mpango mpya wa bima ya afya hadi chini ya wabunge 22 miongoni mwa wabunge wao 237 katika bunge la jumla ya wabunge 430.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri:Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com