Trump arudisha nyuma baadhi ya sera za Obama kwa Cuba | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Trump abadili baadhi ya sera za Obama kwa Cuba

Trump arudisha nyuma baadhi ya sera za Obama kwa Cuba

Wakati uamuzi wa Rais Doland Trump wa Marekani wa kubadili baadhi ya sera za maridhiano na Cuba umewagawa wabunge wa chama chake cha Republikan umeshutumiwa na Cuba kwa kuimarisha vikwazo vya usafiri na biashara.

Wakati wahafidhina wanaompinga Castro wamekaribisha hatua za kurudisha nyuma baadhi ya sera za maridhiano za aliyekuwa rais Barack Obama na Cuba wabunge kadhaa wa chama cha Republikan hususan kutoka majimbo ya kilimo wamekosowa mabadiliko hayo kuwa ni potofu na ya kujitenga.Wamemtaka rais aregeze vizingiti kati ya nchi hiyo na Cuba ili kukuza biashara na kuzalisha ajira kwa nchi zote mbili.

Mbunge wa chama hicho Rick Crawford wa jimbo  la R-Ark amesema mabadiliko hayo ya Trump yatakuwa na madhara zaidi mbali na kuppoteza fursa kwa eneo la vijiji la Marekani ambalo lingefaidika na kwa kupata nafasi kubwa zaidi ya kuingiza bidhaa katika soko la kilimo la Cuba.

Amesema sera ya Trump yumkini ikauweka hatarini usalama wa taifa wakati washindani muhimu wakichukuwa hatua ya kuziba pengo hilo.

Crawford ameongeza kusema kutojihusisha huko zaidi kwa Marekani kunafunguwa fursa kwa nchi nyengine kama vile Iran,Urusi,Korea Kaskazini na China kujipatia ushawishi kwa kisiwa hicho kilioko maili 90 nje ya mwambao wa Marekani.

Maslahi kwa nchi zote mbili

Kuba - Tourismus - USA (Getty Images/AFP/A. Roque)

Meli ya kwanza ya kitalii ikiwasili Cuba kutoka Marekani baada ya miongo kadhaa.

Naye seneta Jeff Flake wa R-Ariz ambae alikuwa akimkosowa Trump mara kwa mara wakati wa kampeni za urais mwaka 2016 amesema katika taarifa kwamba sera yoyote ile ambayo inapunguza uwezo wa Wamarekani kusafiri huru kwenda Cuba haina maslahi kwa Marekani au kwa wananchi wa Cuba.

Flake alikuwa miongoni mwa wabunge wakosoaji wakubwa kabisa wanaopinga kurudishwa nyuma kwa hatua za Obama kupatana na Cuba.Ameonya kwamba kurudi katika sera za kuiwekea ngumu Cuba kunamuumiza kila Mcuba ambaye maisha yake yanazidi kutegemea shughuli za usafiri na utalii.

Katika taarifa yake Flake ametowa wito kwa uongozi wa kamati ya seneti kuruhusu muswada huo kupigiwa kura ambao amesema utaondowa taratibu za vurugu kwa safari za kwenda Cuba ambazo haziko kwa safari za Wamarekani kwenda katika nchi yoyote ile duniani.Muswada huo una wadhamini wenza 54 wakiwemo wabunge tisa wa Republikan.

Cuba yashutumu Marekani

Kuba - Tourismus - USA (Getty Images/AFP/Y. Lage)

Watalii wa Marekani mjini Havana, Cuba.

Cuba hapo Ijumaa imeshutumu hatua ya Rais Doland Trump kurudisha nyuma kile alichokiita "makubaliano ya upande mmoja kabisa ya utawala wa Obama na Cuba."

Serikali imesema katika taarifa yake kupitia televisheni ya taifa kwamba inashutumu hatua hizo mpya za kuimarisha vikwazo ambazo zitashindwa.Hata hivyo serikali hiyo ya Cuba pia imesisitiza kuwa tayari kwake kuendelea na mazungumzo ya heshima na ushirikiano kwa masuala ya maslahi ya nchi hizo mbili.

Mapema hapo Ijumaa Trump amesema anafuta makubaliano ya mtangulizi wake Barack Obama na kisiwa hicho cha Kikoministi ambacho kimerudisha uhusiano wa kibalozi baada ya miaka hamsini.

Trump amewaambia Wamarekani wenye asili ya Cuba huko Miami kwamba atabana baadhi ya vikwazo vya safari na biashara na Cuba juu ya kwamba ameziachilia bila ya kuzigusa hatua za mageuzi mbali mbali yalioachwa na Obama.

Trump ametowa wito wa kufanyika mbadiliko nchini Cuba ikiwa ni pamoja na kuachiliwa huru kwa wafungwa wa kisiasa,kuitisha uchaguzi huru na wa haki na kuheshimu uhuru wa kuzungumza na wa kukusanyika.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/dpa

Mhariri: Yusra Buwayhid

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com