1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump agoma kuhudhuria kikao cha uchunguzi dhidi yake

Daniel Gakuba
2 Desemba 2019

Ripoti ya Baraza la Wawakilishi la Marekani kuhusu mchakato wa kumchunguza Rais Donald Trump itawasilishwa leo katika kikao cha faragha. Ikulu ya White House imekataa mwaliko wa kushiriki.

https://p.dw.com/p/3U4G1
USA Präsident Donald Trump
Picha: imago images/UPI Photo/Y. Gripas

Kamati ya masuala ya kijasusi katika Baraza la Wawakilishi ambayo inadhibitiwa na wabunge wa chama cha Democratic, imesema ripoti hiyo iliyoandikwa kutokana na ushahidi uliotolewa kwa wiki kadhaa itazungumza yenyewe, katika kubainisha kile mwenyekiti wa kamati hiyo, Adam Schiff alichokiita ''makosa na ukosefu wa maadili'' vilivyofanywa na Rais Trump katika matendo yake kuhusiana na Ukraine.

Wabunge ambao ni wanachama wa kamati hiyo watakuwa na fursa ya kuipitia ripoti hiyo, kabla ya kuipeleka katika kamati ya masuala ya kimahakama kesho Jumanne.

Uchunguzi wa ''majuha''

Streit um Mueller-Bericht : Kongresskammer erlaubt rechtliche Schritte gegen Trump-Regierung
Wanachama wa Kamati ya Masuala ya Kijasusi, Bunge la MarekaniPicha: picture-alliance/AP Photo/J. S. Applewhite

Muda mfupi uliopita wakili wa Ikulu ya White House Pat Cippllone amesema Ikulu hiyo haitashiriki katika kikao cha kamati hiyo ya masuala ya mahakama Jumatano ijayo, akikosoa vikali alichokiita ''uchunguzi usio na msingi na unaofuata msingi wa kivyama''. Rais Donald Trump mwenyewe amekemea kwa maneno makali, hatua iliyofikiwa katika uchunguzi dhidi yake.

Amesema, ''Na wendawazimu wale wale wanaendeleza mchakato uliochanganyikiwa, wa kunichunguza, kama mwanzo. Na wanausukuma mchakato huo, ambao ni kama kumuinda mchawi, na mambo mabaya yanatokea upande wao. Mnaona uchunguzi wa maoni? Kila mtu anasema, haya ni bure kabisa''.

Jerry Nadler US-amerikanischer Politiker
Mwenyekiti wa kamati ya masuala ya kimahakama katika bunge la Marekani, Jerrod NadlerPicha: picture-alliance/newscom/K. Dietsch

Wakili wa Ikulu ya White House, Pat Cipollone amesema katika barua aliyomtumia mwenyekiti wa kamati ya masuala ya kimahakama Jerrod Nadler ambaye ni Mdemocrat, kwamba mchakato wa kumchunguza Rais Trump unakiuka mifano yote ya awali, ilikuwa na misingi ya haki. Rais Trump mwenyewe, siku ya Jumatano atakuwa mjini London, akihudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Mwenendo wa hatari

Jerrod Nadler amesema mwenendo wa ofisi ya Rais Trump wa kutaka kumkingia kifua, ni wenye hatari kubwa.

''Ikulu ya White House inaendekeza nadharia mpya tena ya hatari sana. Ni mbaya kupita kinga ya jumla jamala. Mpaka uko wapi? Ni kuzia haki, hakuna zaidi ya hapo.'' na kuendelea, '' Ikiendelea, na hususan uhusikapo uchunguzi wa kamati ya kimahakama juu ya kipengele cha kumfungulia mashtaka rais, itavuruga ugawanaji wa madaraka kama ulivyowekwa na watangulizi wetu.''

Wakati mchakato huu wa uchunguzi dhidi ya Trump ukiendelea kushika kasi, kikao cha Jumatano kitakuwa chenye umuhimu mkubwa, kwani kitawaleta pamoja wataalamu wa masuala ya sheria, ambao ushahidi wao, pamoja na ripoti ya kamati ya masuala ya kijasusi, vitaweka msingi wa uwezekano wa kipengele cha kumshitaki rais, ambacho jopo linatarajiwa kuanza kukiandika hivi karibuni.

 

ape, afpe