1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wademocrat wambwagia lawama Trump kwa mauaji

5 Agosti 2019

Wagombea wa Urais wa chama cha Democratic nchini Marekani wamemlaumu Rais Donald Trump kufuatia visa viwili vya mashambulizi ya bunduki vilivyosababisha vifo vya watu 29 huko Texas na Ohio.

https://p.dw.com/p/3NLmu
USA Texas | Trauer nach der Schießerei in einem Supermarkt in El Paso
Picha: Reuters/C. Sanchez

Wagombea hao wanasema matamshi ya Trump ya kibaguzi dhidi ya walio wachache nchini humo yanachochea mgawanyiko na machafuko.

Katika mikutano ya umma na hata kwenye televisheni wagombea kadhaa wamezungumzia haja ya kuwepo kwa sheria kali za udhibiti wa bunduki. Lakini wanasiasa hao wameelekeza kiasi kikubwa cha lawama zao kwa Trump wakisema mashambulizi hayo ya Dayton na El Paso yana uhusiano na matamshi yake ambayo amekuwa akiyatoa kwa miezi sasa dhidi ya wahamiaji na watu watu wasio wazungu.

Seneta Bernie Sanders amesema na hapa namnukuu "namwambia Rais Trump, tafadhali achana na matamshi ya kibaguzi dhidi ya wahamiaji, wachana na chuki inayoshuhudia nchi hii ikitumbukia katika machafuko tunayoyaona."

Trump asema utawala wake umefanya juhudi kubwa mno

Rais Trump mwenyewe amelaani mashambulizi yote mawili, "ninachotaka kusema ni kwamba hizi ni sehemu mbili nzuri na tunawapenda watu wake. Chuki haina nafasi katika nchi yetu na tutalishughulikia suala hilo," alisema Trump.

USA nach Anschlägen | Donald Trump, Präsident & Ehefrau Melania in Morristown
Rais Trump anasema utawala wake umefanya mengiPicha: Reuters/Y. Gripas

Alipoulizwa kuhusiana na hatua atakazochukua baada ya tukio hilo la mauaji, Trump alisema;

"Tumefanya mengi zaidi kuliko tawala zilizopita na jambo hilo halizungumziwi sana, lakini tumefanya mengi kusema kweli. Lakini labda mengi zaidi yanastahili kufanyika."

Watu ishirini waliuwawa katika duka la jumla la Walmat mjini El Paso huko Texas na polisi inasema kisa hicho kitachukuliwa kama ugaidi wa ndani ya nchi wakati ambapo wanachunguza madai ya shambulizi lililotokana na chuki ambapo huenda mshukiwa akahukumiwa kifo iwapo atapatikana na hatia. Polisi pia inasema haijui bunduki hiyo iliponunuliwa ingawa inasema pia kuwa sheria huko Texas inakubali kubeba bunduki kubwa katika sehemu ya umma.

Mshukiwa aliwahi kusimamishwa shule kwa kuwa na orodha ya watu anaotaka kuwauwa

Mexico kupitia waziri wake wa mambo ya nje imesema inapanga kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu aliyemuuzia mshambuliaji huyo silaha kwani raia sita wa Mexico ni miongoni mwa waliouwawa.

USA Texas | Trauer nach der Schießerei in einem Supermarkt in El Paso
Ilikuwa ni vilio huko Texas baada ya shambuliziPicha: Reuters/J. Luis Gonzalez

Aliyefanya shambulizi la Dayton Ohio aliuwawa na polisi. 

Hayo yakiarifiwa wanafunzi waliokuwa darasa moja na kijana aliyefanya shambulizi la huko Ohio wanasema kuna wakati alifukuzwa shule baada ya kuandika orodha ya watu anaotaka kuwauwa na orodha nyengine ya wasichana anaonuia kuwabaka.

Kauli hizo za wanafunzi hao zimekuja baada ya polisi kusema kuwa hakukuwa na taarifa yoyote mbaya ambayo ingeweza kumzuia mshukiwa Connor Betts kununua silaha hiyo aliyoitumia kufyatua risasi nje ya baa iliyokuwa imejaa watu.