1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump afikiria kuwania tena Urais 2024

1 Machi 2021

Akionekana kwa mara ya kwanza kwa umma tangu aondoke madarakani, aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump ameweka wazi uwezekano wa kuwania tena Urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2024.

https://p.dw.com/p/3q2fv
USA | Florida | Donald Trump hält eine Rede bei der US-Republikanertreffen CPAC in Orlando
Picha: Joe Skipper/REUTERS

Akizungumza katika mkutano wa kisiasa wa muungano wa kihafidhina CPAC uliofanyika mjini Orlando katika jimbo la Florida, mwanachama huyo wa Republican amesema huenda akajitosa katika kinya'nganyiro cha Urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Akiashiria uwezekano huo, Trump aliyeiongoza Marekani kwa muhula mmoja kuanzia mwaka 2017 hadi 2021 amesema:

"Nani anayejua. Ninaweza kuamua kuwashinda kwa mara ya tatu. Hio ni sawa?

Trump pia amesisitiza madai yake yasiokuwa na ushahidi kuwa alimshinda rais wa sasa Joe Biden katika uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka uliopita.

Rais huyo wa zamani ambaye amehamia katika makaazi yake ya Mar-a-Lago katika jimbo la Florida baada ya kuondoka Ikulu mnamo Januari 20, amerudia madai yake juu ya uchaguzi ulioibiwa na mara kwa mara amekataa kukubali kushindwa.

Trump anadai kuwa uchaguzi wa mwezi Novemba ulikumbwa na udanganyifu mkubwa lakini hajawahi kutoa ushahidi wowote kuunga mkono madai yake.

Trump pia alikataa wito wa kuanzishwa kwa chama kipya cha kisiasa. Alipuzilia mbali ripoti za uwezekano wa kuanzishwa kwa chama cha Trump akizitaja kama habari za uwongo.

"Tukiwa pamoja katika miaka ijayo, tutaubeba na kuupeleka mbele mwenge wa uhuru wa Marekani. Tutaongoza harakati za kihafidhina na chama cha Republican kurudi kwenye ushindi kamili. Na tumewahi kupata ushindi mkubwa. Musisahau kamwe"

Trump akosoa sera za Biden

USA | US-Republikanertreffen CPAC| Donald Trump hält eine Rede in Florida
Picha: Octavio Jones/REUTERS

Trump pia amekosoa vikali sera za Biden, hatua ambayo sio kawaida kwa rais wa zamani wa Marekani ambaye ameondoka ofisini hivi karibuni.

Rais huyo wa zamani amedai kuwa Biden amekuwa na mwezi wa kwanza mbaya katika utawala wake kwenye historia ya nchi hiyo na kumshtumu Rais huyo wa sasa kwa kutaka kuifanya Marekani kuwa "nchi ya ujamaa"

Donald Trump bado ana ufuasi mkubwa ndani ya chama chake cha Republican. Katika kura isiyokuwa rasmi ya muungano wa kihafidhina CPAC, asilimia 95 waliunga mkono muendelezo wa sera za Trump huku asilimia 70 wakitaka Trump awanie tena Urais katika uchaguzi wa mwaka 2024.

Hata hivyo wakosoaji wake hawakuhudhuria mkutano huo.

Mkutano huo wa kila mwaka hufanyika mjini Washington lakini ulihamishwa hadi Orlando kutokana na vizuizi vya Covid-19 vilivyowekwa mjini Florida.