1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Taytu Betul: Malika wa Ethiopia mke wa Menelik II

Yusra Buwayhid
22 Februari 2021

Taytu Betul, alikuwa ni mke wa mfalme Menelik wa Pili ni mmoja wa viongozi shupavu wa Ethiopia. Alichangia kuvishinda vikosi vya Italia, ilipojaribu kuitawala Ethiopia, na ndiye aliyetoa jina la mji mkuu wa Addis Ababa.

https://p.dw.com/p/3phph

Taytu Betul: Malkia wa Ethiopia mke wa Menelik II

Ni nani Taytu Betul?

Taytu Betul alikuwa ni mwanamke mashuhuri kutoka Ethiopia. Pamoja na mume wake Mfalme Mkuu Menelik II, waliitawala Ethiopia kutoka mwaka 1889 hadi 1913. Anakumbukwa kwa upinzani wake dhidi ya wanajeshi wa kikoloni wa Italia, na uwezo wake mkubwa wa kisiasa. Pia ndiye aliyelichagua eneo ulipo leo hii mji mkuu wa Ethiopia na kuupa jina la Addis Ababa.

Taytu Betul alikuwa nani kabla ya kuwa malkia?

Taytu Betul alizaliwa mnamo mwaka 1840 au 1851, katika eneo la Debre Tabor, ambalo haliko mbali na Ziwa Tana. Anatoka katika familia mashuhuri na yenye ushawishi inayodai asili ya ukoo wake ni Mfalme Suleiman na Malkia Sheba. Aliolewa kwa mara ya kwanza akiwa na umri mdogo wa miaka kumi, kitu ambacho kilikuwa kawaida kwa mtoto wa kike anayetoka familia mashuhuri. Inasemekana ndoa zake nyingi hazikuwa na furaha, na hatimaye aliolewa kwa mara ya tano na Mfalme Menelik II. Wakati wa ndoa yake hiyo, alikuwa tayari ameshajikusanyia utajiri na mali ya kutosha.

Je, Taytu Betul alipataje nguvu?

Ndoa yake na Menelik alikuw ana nguvu kubwa ya kisiasa, baada ya kuziunganisha koo zao mbili. Taytu Betul ametokea kaskazini na Menelik ametokea kusini mwa Ethiopia. Baada ya kuoana na mfalme huyo na malkia wake walitafuta ushirikiano na makabila mengine tofauti ya Ethiopia. Walitumia uhodari wao wa kisiasa pia na walikuwa na nguvu ya kijeshi iliyowasaidia kufanikiwa.

African Roots | Taytu Betul
Asili ya Afrika | Taytu Betul

Taytu Betul hakutaka tu kuwa malkia wa mfalme. Alihakikisha anashirikishwa katika kufanya maamuzi yote ya kisiasa, kidiplomasia pamoja na katika kuamua mikakati ya kijeshi. Wanahistoria wanasema alikuwa na ushawishi sawa na mume wake, na wakati mwengine akionekana kuwa na misimamo mikali zaidi kuliko hata mfalme Menelik.

Taytul Betul anakumbukwa zaidi kwa lipi?

Taytul Betul anakumbukwa zaidi kwa umahiri wake aliouonesha wakati wa vita vya Adwa ambapo Ethiopia ilipambana dhidi ya Italia. Taytu inasemekana aliongoza kikosi kilichokuwa na wanajeshi 5,000 waliokuwa hawana farasi na wengine 600 waliokuwa juu ya farasi, na kupigana na Wataliana waliokuwa wakijaribu kuivamia na kuitawala Ethiopia. Taytu alipinga vikali kuingia mikataba na Italia na iliupinga hasa Mkataba wa Wuchale, ambao ulitaka kuiweka Ethiopia chini ya ulinzi wa Italia kama mkoloni. Taytu alikuwa miongoni mwa walioamrisha mikakati ya mashambulizi wakati wa vita na Italia. Alisimama mstari wa mbele na kuongoza kikosi cha wanajeshi. Na alipata ushindi mkubwa katika ngome iliyojengwa na Wataliana huko Mekelle, baada ya kuwafungia usambazaji wa maji.

Taytu Betul: Malkia wa Ethiopia aliyewashinda Wataliana

Je, Taytu alikuwa ni mwanamke wa ajabu kwa wakati huo?

Wanawake wa Ethiopia wa wakati huo walikuwa na nguvu kwa kiasi. Wake na mama wa wafalme na wanawake wengine wengi walikuwa wakiongozana na vikosi vya wanajeshi wakati wa vita. Lakini hawakuwa wakibeba silaha. Mchango wao mkuu ulikuwa ni kuwasaidia wanajeshi wanapojeruhiwa, kuwapikia na kuwasafishia.

Ilikuwa kitu cha nadra kwa mwanamke kuongoza kikosi kizima cha wanajeshi vitani kama alivyothubutu kufanya Taytu. Katika baadhi ya michoro inayoonyesha Vita vya Adwa, anaonekana kati kati ya mapigano. Hata hivyo, hakuna ushahidi wowote unaomuonyesha akiwa amebeba silaha. Alikuwa mwananmke anayeweza kusoma na kuandika, na hilo lilifanya aonekane kama mwanamke wa kipekee. Taytu pia alipenda kucheza mchezo wa chess, akipenda muziki, na akijua kucheza ala ya muziki iitwayo Begena.

Nini kilitokea baada ya kifo cha Menelik?

Mnamo mwaka 1909 Menelik alipata ugonjwa wa kiharusi, na Taytu alikamata hatamu ya utawala, na kuiongoza Ethiopia kwa ufanisi mkubwa. Baada ya muda, wapinzani wake katika familia ya kifalme walimshinikiza kuachia madaraka. Wanahistoria wanasema alikuwa na nguvu sana iliyowatisha baadhi ya watu waliokuwa wamemzunguka.

Menelik alipofariki mwaka 1913, Taytu alitengwa kutoka katika kasri kuu, na ushawishi wake wa kisiasa ukafifia. Alifariki dunia mnamo mwaka 1917.

Vipi tumeweza kujua yote haya kuhusu Taytu Betul?

Tumeweza kujua mengi kuhusu Taytu Betul kupitia fasihi simulizi pamoja na rekodi za nyaraka na michoro ya kale. Watu waliokuwa sehemu ya kasri la mfalme wa Ethiopia, wanadiplomasia wa kigeni, wafungwa wa Wataliana waliokuwa wafungwa wa kivita, na hata baru alizoziandika mwenye Betul; yote haya yametupa maelezo ya kina juu ya malkia huyu wa Ethiopia.

Mhandisi wa Uswisi, Alfred Ilg, ambaye alifanya kazi kwenye kasri la mfalme Menelik na malkia Taytu aliwapiga picha ambazo pia zinaonyesha jinsi maisha walivyokuwa wakiishi maisha yao ya kifalme.

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.