1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yatoa tahadhari ya Mafua Makali, UVIKO-19

25 Februari 2026

Wizara ya Afya nchini Tanzania imetoa tahadhari ya kuwepo na ongezeko la wagonjwa wa mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 na vilevile homa ya Dengue na Kipindupindu.

https://p.dw.com/p/59Njv
Tanzania Dar es Salaam wakati wa Uviko-19, 2020
Miongoni mwa wakaazi wa Dar es saalam aliyevalia barakoa wakati wa mlipuko wa UVIKO 19 mwaka 2020Picha: DW/E. Boniphace

Taarifa iliyotolewa Jumatano 25 Februari na Mganga Mkuu wa serikali ya Tanzania Dkt. Grace E. Magembe, imesema kwamba takwimu za ufuatiliaji zinaonesha kuwa, kila mwaka katika kipindi cha mwezi Novemba hadi Aprili kunakuwa na ongezeko la ugonjwa wa mafua makali ya Influenza na UVIKO19 nchini humo na duniani.

Njia zinazoeneza magonjwa hayo

Kulingana na Dkt. Magembe, magonjwa haya huenezwa kupitia majimaji kutoka kwenye mfumo wa njia ya hewa wa mgonjwa mwenye maambukizi na husambaa wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuzungumza.

Vilevile, mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 huweza kuenezwa kwa kugusa mazingira yaliyochafuliwa na majimaji yanayotoka kwa mgonjwa. Dalili za magonjwa haya ni homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua, kuwashwa koo na uchovu.

Tanzania Dar es Salaam | Michoro ya kuelemisha namna ya kujikinga na Corona
Mchoro wa grafiti ukihimiza namna ya kujikinga na maambukizi ya Corona jijini Dar es salaamPicha: Eric Boniphace/DW

Nini cha kufanya ili kuchukua tahadhari

Wizara ya afya ya Tanzania imewataka wanachi kuchukua tahadhari ya namna ya kujikinga na magonjwa hayo kwa kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono, kuepuka misongamano isiyo ya lazima.

Pia imewataka watu kuvaa barakoa wanapokuwa na dalili, wanapokuwa karibu na mtu mwenye dalili au wakiwa kwenye maeneo yenye msongamano, kuzingatia usafi binafsi na wa mazingira, kuwahi katika kituo cha kutolea huduma za afya kupata matibabu stahiki, vile vile kuepuka kujitibu au kutumia Antibiotiki bila ushauri wa wataalam wa afya.

Tahadhari ya Homa ya Dengue na mlipuko wa kipindupindu

Taarifa ya Mganga Mkuu pia imetahadharisha juu ya ugonjwa wa Homa ya Dengue kutokana na maeneo mengi kuwa katika kipindi cha mvua za masika zinazopelekea kuongezeka kwa mazalia ya mbu.

Athari za homa ya dengue Tanzania

Homa ya Dengue huenezwa na mbu aina ya Aedes ambaye ni mweusi mwenye madoa doa meupe na hupendelea kuuma nyakati za asubuhi, mchana na jioni.

Kulingana na Mganga Mkuu, Tanzania imekuwa katika mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu ulioathiri mikoa yote isipokuwa Kilimanjaro na Njombe.

“Kwa kipindi cha takriban mwezi mmoja uliopita, nchi yetu haijapata mgonjwa wa Kipindupindu,“ ilisema taarifa hiyo.