1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Suu Kyi kuendelea kuzuiliwa wakati maandamano yakiendelea

Saleh Mwanamilongo
15 Februari 2021

Viongozi wa kijeshi nchini Myanmar wanatuma vikosi zaidi kote nchini ili kukabiliana na maandamano ya raia wanaopinga mapinduzi ya kijeshi.

https://p.dw.com/p/3pN7w
Myanmar Proteste nach Militärputsch in Yangon
Picha: REUTERS

Viongozi wa kijeshi nchini Myanmar wanatuma vikosi zaidi kote nchini ili kukabiliana na maandamano ya raia wanaopinga mapinduzi ya kijeshi. Licha ya vitisho hivyo waandamanaji wamejitokeza tena leo Jumatatu wakiomba kuachiwa huru kwa kiongozi wao Aung San Suu Kyialiyekamatwa pamoja na mamia ya wafuasi wake wengine.

Jeshi linajaribu kuzima maandamano ya raia kufuatia mapinduzi ya kijeshi wiki mbili zilizopita. Waandamanaji walijitokeza kwa uwingi Jumatatu licha ya kufungwa mawasiliano ya intaneti. Vikosi vya ziada pamoja na vifaru vya kijeshi vilionekana leo kwenye barabara kuu za Yangon,mji mkuu wa kibiashara.

Jumuiya ya kimataifa yalaani mapinduzi

Picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii muda mfupi kabla ya kufungwa mawasiliano,zilionyesha magari ya kijeshi pamoja na wanajeshi wakijielekeza kwenye maeneo mengine ya nchi.

Maandamano mapya yazuka jumatatu mjini Yangon na kwenye miji kadhaa ya Myanmar.
Maandamano mapya yazuka jumatatu mjini Yangon na kwenye miji kadhaa ya Myanmar.Picha: AP/picture alliance

Aidha maandamano yaliibuka mjini Yangon, karibu na benki kuu ya taifa. Taarifa za vyombo vya habari zinasema kuwa waandishi habari wasiopungua watano waliokuwa wakifuatilia maandamano hayo walikamatwa.

Balozi za magharibi nchini Myanmar zimewatolea mwito viongozi wa kijeshi nchini humo kujizuia na matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji na raia. Balozi za Umoja wa Ulaya, Uingereza, Canada na nyingine 11 pia zimelaani kamatakamata ya viongozi wa upinzani na manyanyaso dhidi ya waandishi wa habari baada ya mapinduzi ya Februari Mosi. Kwenye taarifa yao wamesema wanaunga mkono madai ya raia wa Myanmar ya demokrasia, uhuru, amani na utulivu na kuongeza kuwa dunia inatazama.

Afisa maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar, Tom Andrews kupitia ukurasa wa twitter ameandika hizi ni dalili za kukata tamaa huku akiwaonya majenerali walioongoza mapinduzi hayo kuwa watawajibishwa kwa hatua zao.  

Suu Kyi kubaki rumande hadi Februari 17

Wakati huo huo, viongozi wa jeshi wameongeza muda wa kumzuia kiongozi aliyeondolewa madarakani Aung San Suu Kyi, muda ambao ulitarajiwa kukamilika leo Jumatatu.

Kwa mujibu wa wakili anayemuwakilisha Suu Kyi, Khin Maung Zaw, kiongozi huyo atazuiliwa rumande hadi Februari 17 wakati ambapo huenda akafikishwa kortini na vikao hivyo kuendeshwa kwa njia ya video.

Aung Suu Kyi ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel yuko chini ya kizuizi cha nyumbani kwa shtaka la kuingiza nchini humo redio sita za upepo kinyume cha sheria.