1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan: Omar al Bashir kufikishwa mahakamani wiki ijayo

Zainab Aziz Mhariri: Rashid Chilumba
16 Juni 2019

Mwendesha mashtaka mkuu nchini Sudan amesema kiongozi aliyeondolewa madarakani Omar al-Bashir atafikishwa mahakamani wiki ijayo.

https://p.dw.com/p/3KXGJ
Sudans Präsident Omar al-Bashir
Picha: Getty Images/A. Shazily

Mwendesha mashtaka mkuu Al Waleed Sayyed Ahmed amewaambia waandishi wa habari kwamba Bashir anakabiliwa na mashtaka ya rushwa na kumiliki fedha za kigeni kinyume cha sheria.

Hayo yanatokea baada ya zaidi ya miezi miwili tangu jeshi lilipomwondoa Bashir madarakani kufuatia maandamano makubwa ya kitaifa yaliyopinga utawala wake. Siku ya Alhamisi, afisa mmoja alinukuliwa na shirika la habari la Sudan, SUNA, akisema Bashir  anakabiliwa pia na mashtaka ya kuamuru hali ya dharura nchini Sudan.

Mnamo mwezi Aprili, mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alisema fedha zaidi ya dola milioni 113 zilikamatwa kutoka kwenye makazi ya al-Bashir. Jenerali Burhan amesema polisi na wanajeshi na mawakala wa usalama walipata kiasi cha Euro milioni saba , Dola za Kimarekani 350,000 na Pauni za Sudan milioni moja na tano.

Waandamanaji nchini Sudan
Waandamanaji nchini SudanPicha: AFP/M. El-Shahed

Omar al Bashir alipotangaza hali ya dharura mnamo Februari 22 katika jitihada za kuyazima maandamano yaliyoanza kutoka mwezi Desemba, Bashir alitoa alipitisha amri kwamba ni kinyume cha sheria kwa mtu kuwa na fedha za kigeni zaidi ya dola 5,000.

Mwezi uliopita, mwendesha mashtaka mkuu Ahmed aliamuru Bashir ahojiwe kuhusu tuhuma za utakatishaji fedha na kufadhili ugaidi. Mnamo mwezi Mei, mwendesha mashtaka huyo  alisema Bashir atashtakiwa kwa mauaji ya waandamanaji waliokuwa wanaipinga serikali yake jambo lililosabisha kuondolewa kwake madarakani.

Ahmed amesema watuhumiwa wengine waliotumikia chini ya utawala wa Bashir bado wanachunguzwa.  Ingawa hakuwataja majina lakini alisema tuhuma dhidi yao ni kuhusu umilki wa ardhi.

Maandamano dhidi ya utawala wa Bashir yalianza tarehe 19 Desemba baada ya serikali yake kupandisha bei ya mkate. Omar al Bashir aliondolewa madarakani na jeshi tarehe 11 Aprili baada ya maelfu ya waandamanaji wakiongozwa na muungano wa vyama vya watu stadi kupiga kambi mbele ya makao makuu ya jeshi katikati ya mji mkuu Khartoum kuanzia Aprili 6. Kwa sasa anazuiwa kwenye gereza la Kober.

Chanzo: AFP