Sudan Kusini: Raia 16 wauawa kufuatia vita Wau | Matukio ya Afrika | DW | 11.04.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Mapigano Wau

Sudan Kusini: Raia 16 wauawa kufuatia vita Wau

Watu wasiopungua 16 wanaripotiwa kuuawa na wengine 10 kujeruhiwa Sudan Kusini  kufuatia mapigano makali  katika  mji wa pili kwa ukubwa wa Wau

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS umesema mapigano hayo yalitokana na kuuawa  kwa askari wa jeshi la serikali.SPLA  waliokuwa wakipiga doria eneo hilo la kaskazini mwa Sudan Kusini. Karibu  nusu ya mji huo wa Wau imesalia kimya huku maduka na hata masoko yakifungwa kufuatia  tangazo la serikali la kuwataka wenyeji kusalia majumbani mwao. Ujumbe wa UNMISS umesema watu 84 wametafuta hifadhi katika kambi ya kuwalinda raia ya  Umoja  wa Mataifa  huku wengine wapatao elfu tatu wakipewa hifadhi  katika kanisa  moja la katoliki  lililo katika mji huo wa Wau baada ya kuhofia usalama

Südsudan Flüchtlinge suchen Schutz UN-Mission in Juba (picture-alliance/dpa/UNMISS/E. Kanalstein)

Akinamama na watoto katika kambi ya kuwalinda raia ya UN

wao. Kwa mujibu wa mmoja wa  wakaazi; idadi ya waliofariki huenda ikiwa juu kuliko ilivyoripotiwa na waliolengwa hasa ni kutoka  makabila ya wachache ya Jur na Balanda  wanaodaiwa kuwaunga mkono waasi. Mji huo wa Wau umo katika eneo ambalo limeshuhudia mara kadhaa ubadilishanaji udhibiti kati ya vikosi vya serikali  na waasi wanaomuunga mkono aliyekuwa makamu wa rais  Riek Machar tangu kuzuka mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013. Hata hivyo mji wenyewe miaka yote umesalia chini ya usimamizi wa wanamuuunga mkono rais Salva Kiir. Ujumbe wa UNMISS umesema wiki iliyopita kuwa vikosi vya serikali vilisafirisha vifaa vyao na magari ya kijeshi  katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi  kusini mashariki mwa mji huo wa Wau.

Taarifa zinazohitilafiana

Msemaji wa kijeshi Santo Choi  amesema mapigano hayo yanatokana vikosi vyake kuanzisha harakati za kuwatimua waasi  kutoka eneo hilo  ambalo ni ngome yao kwa muda mrefu.Nae msemaji wa waasi  William Deng  amesema vurugu za sasa zilitokana na uvamizi waliofanya dhidi ya vikosi vya serikali  siku ya jumapili ambapo 35 miongoni mwao walifariki.

Südsudan Juba SPLA-IO Soldaten (picture-alliance/AP Photo/J. Patinkin)

Kikosi vya aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar

Katika kulipiza kisasi msemaji huyo wa waasi amesema majeshi ya serikali yalirejea katika mji huo wa Wau ambapo walifanya msako wa nyumba kwa nyumba na kuwaua raia 50. Taarifa  hizo kutoka kwa serikali na waasi bado hazijathibitishwa. Viongozi wa South Sudan  walipigania uhuru miongo kadhaa, lakini tangu kuupata uhuru huo mwaka 2011 mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yalianza  mwaka 2013 kufuatia mapambano ya kuwania uongozi kati ya rais Kiir na aliyekuwa makamu wake Riek Machar. Watu wapatao millioni 1.7 wametoroka Sudan Kusini  tangu taifa hilo kutumbukia katika vita huku  wengine millioni 1.9  wakisalia  wakimbizi wa ndani. Mapigano hayo  pia yamesababisha ukame na kuchochea mgogoro wa kibinadamu. 

Mwandishi:Jane Nyingi/AFPE
Mhariri:Iddi Ssessanga