1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Suala la uraia wa Marekani kutishia sensa 2020

Yusra Buwayhid
7 Februari 2018

Marekani inajiandaa kufanya sensa ya watu mwaka 2020 lakini suala la uraia limezua utata kabla sensa hiyo kuanza. Utaratibu huo utakapoanza, wafanyakazi wa sensa watalazimika kuwauliza watu kama wana uraia wa Marekani.

https://p.dw.com/p/2sDym
USA Washington Donald Trump
Picha: picture-alliance/AP Images/E. Vucci

Arturo Vargas, mkuu wa Mfuko wa Fedha wa Elimu wa NALEO amesema utafiti wa majaribo wa tokea mwezi Septemba unaonesha kwamba watu wamekuwa na hofu dhidi ya serikali ya Marekani kwa kiwango ambacho hakikuwahi kutokea.

Rais wa Marekani Donald Trump amechukua hatamu ya uongozi kwa kutumia ajenda ya kitaifa ya kupambana na wahamiaji, kuwahusisha wageni na wahamiaji nchini nchini humo na magaidi, uhalifu na ukosefu wa ajira. Katika hotuba yake ya mwezi uliopita, amerudia ahadi yake ya kupunguza uhamiaji.

Wataalamu  wa  masuala ya  kijamii  wanasema katika hali hiyo, huku kukiwa na ripoti za mara kwa mara za wahamiaji kutenganishwa na familia zao na kurejeshwa walipotoka, idadi kubwa ya watu nchini Marekani watakataa kushiriki katika sensa hiyo, kwa hofu kwamba serikali inaweza kutumia taarifa watakazozitoa dhidi yao.

Mwezi Desemba Idara ya Sheria ilizua mzozo pale ilipotaka suala la uraia lijumuishwe katika orodha ya masuala ya utafiti huo wa sensa unaosimamiwa na Ofisi ya Sensa, ambayo ni sehemu ya Idara ya Biashara.

Idara ya Sheria imesema kuwa taarifa za uraia zitasaidia kutekeleza Sheria ya Haki za Upigaji kura, hata hivyo sheria hiyo inalenga kuzuia ubaguzi wa rangi  wakati wa  kupiga  kura. Raia wa Marekani tu ndio wanaruhusiwa kujiandikisha ili kupiga kura. Lakini Trump kwa muda mrefu amekuwa akidai kwamba mamilioni ya wahamiaji haramu walipiga kura katika uchaguzi wa rais wa 2016, bila kutoa ushahidi.

Orodha kukamilika Machi 31

Al Fontenot, mkurugenzi mshiriki wa programu za sensa amesema wanatarajia kuwa na orodha ya mwisho ya maswali yaliyowasilishwa katika Baraza la Congress ifikapo Machi 31.

USA Kapitol in Washington
Orodha kuwasilishwa kwa baraza la bunge la MarekaniPicha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Mjadala juu ya maswali na jinsi yanavyoweza kuathiri idadi ya majibu sio tu wa kisiasa. Sensa inalazimika kufanywa kulingana na Katiba. Sensa huamua idadi ya viti vilizotengwa kwa kila jimbo katika Braza la Wawakilishi. Mwanasoshololojia wa Stanford Profesa C. Matthew Snipp, amesema utafiti huo ni muhimu kwa demokrasia ya Marekani.

Kulingana na ofisi ya sensa, idadi ya watu pia huathiri usambazaji wa zaidi ya dola bilioni 675,  fedha za shirikisho za kila mwaka kwa shule, hospitali, barabara na huduma za umma.

Kukosea idadi ya watu katika baadhi ya jamii ni tatizo la muda mrefu. Wachambuzi wanakadiria kuwa Sensa ya 2010 ilikosea idadi ya Walatino na kuwapunguza idadi kwa watu 775,000. Tatizo linaweza kuwa baya zaidi mara hii.

Vargas amesema sensa yenye makosa pia inaweza kuwa na athari za kiuchumi na kifedha. Wafanyabiashara hutumia uchunguzi wa huo wa miaka kumi kutambua mwenendo na tabia za watu na kuwalenga wateja na wafanyakazi wenye uwezo, kuwawezesha kupanga vizuri masuala ya uwekezaji, kufanya mipango ya viwanda na maduka ya rejareja, na kuzishawishi benki kuwapa mikopo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe

Mhariri: Sekione Kitojo