1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHong Kong

Sheria mpya ya usalama Hong Kong yaanza kutumika kuanzia leo

23 Machi 2024

Sheria mpya ya usalama wa kitaifa ya Hong Kong imeanza kutumika kuanzia leo, na kuweka adhabu kali ikiwemo kifungo cha maisha gerezani kwa makosa ya uhalifu.

https://p.dw.com/p/4e35r
Kiongozi wa kisiwa cha Hong Kong John Lee
Kiongozi wa kisiwa cha Hong Kong John LeePicha: Hong Kong Information Service Department

Sheria hiyo - inayojulikana kama kifungu cha 23 - inalenga makosa ya aina tano ya usalama wa kitaifa na ilipitishwa kwa kauli moja na wabunge wa Hong Kong siku ya Jumanne.

Marekani, Umoja wa Ulaya, Japan na Uingereza ni miongoni mwa mataifa yalioikosoa sheria hiyo ya usalama wa kitaifa huku waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Cameron akisema sheria hiyo itabinya zaidi haki na uhuru wa raia wa Hong Kong.

Soma pia: Wabunge Hong-Kong wapitisha sheria mpya ya usalama

Kiongozi wa kisiwa hicho John Lee ametaja hatua ya kupitishwa kwa sheria hiyo ya usalama wa taifa kama "wakati wa kihistoria."

Chini ya sheria hiyo mpya, kutatolewa adhabu ya hadi kifungo cha maisha gerezani kwa mtu yeyote anayehatarisha usalama wa taifa, uhaini au kuchochea uasi, miaka 20 jela kwa ujasusi na hujuma, miaka 14 jela kwa kosa la uingiliaji wa nje - kushirikiana na watu wa nje ya kisiwa hicho kwa njia zisizofaa.