Serikali ya Lebanon yapitisha mpango wa mageuzi kutuliza maandamano | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.10.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Serikali ya Lebanon yapitisha mpango wa mageuzi kutuliza maandamano

Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri amesema Baraza lake la mawaziri limeidhinisha mabadiliko kadhaa ya kiuchumi na kukubaliana kuhusu bajeti ya mwaka 2020.

Waziri Mkuu huyo wa Lebanon Saad Hariri akizungumza kupitia televisheni ya kitaifa, amesema mikakati ya kiuchumi na bajeti ya mwaka 2020 kama ilivyokubalika na Baraza lake la mawaziri havilengi kuyasitisha maandamano makubwa yanayoendelea. Hariri amesema uamuzi walioufanya hii leo sio wa kuwataka wananchi waache kuelezea hasira zao.

"Uamuzi huu sio wa kuwafanya muondoke barabarani au kuacha kuelezea matatizo yenu hilo ni jambo mtakaloamua wenyewe na wala sitakubali mtu yeyote kuwatisha. Nataka mujue kilio chenu kinasikika na kama munataka uchaguzi wa mapema basi mimi Saad Hariri nitawaunga mkono kwa hilo,” alisema Saad Hariri.

Serikali hiyo pia imeidhinisha wabunge na mawaziri kupunguziwa nusu ya mishahara yao kama njia moja ya mabadiliko hayo ya kiuchumi, na kutoa wito wa kubinafsisha sekta za umeme na mawasiliano pamoja na kuwa na sheria mpya ya kuzuwiya ubadhirifu wa fedha za serikali.

Hariri ameongeza kuwa Sekta ya benki  itachangia kupunguza nakisi ya fedha kwa pauni trilioni 5.1 za Lebanon sawa na dola bilioni 3.4 ikiwemo kuongeza ushuru kwa faida za benki

Waandamanaji waapa kuendelea na maamndamano yao hadi serikali nzima itakapojiuzulu

Libanon Vierter Tag mit Protesten - «Wir vertrauen euch nicht»

Baadhi ya waandamanaji mjini Beirut

Tamko hili linatokea wakati, maelfu ya raia wa Lebanon wanashiriki maadnamano kwa siku ya tano sasa dhidi ya serikali kushindwa kuimarisha hali ya kiuchumi. Hata hivyo tangazo la Hariri halikulainisha nyoyo za waandamanji wanaotaka serikali nzima ijiuzulu kwa madai ya kuharibu fedha za umma na kutowekeza vya kutosha katika masuala ya afya na mipango ya kijamii.

Baadhi ya waandamanaji waliokuwa wamekusanyika katika uwanja wa Riad al Solh, walimfokea  Kiongozi mwenye ushawishi mkubwa wa chama cha Hezbollah Hassan Nasrallah na kumtuhumu kuiendesha nchi kupitia washirika wake wa karibu ambaye ni rais Michel Aoun.

Hii leo ndio ilikuwa muda wa mwisho aliojiwekea waziri Mkuu Hariri kutaka serikali kupata suluhu ya kiuchumi bila ya kupandisha kodi akitumai mipango yake hiyo itayapoza maandamano makubwa dhidi ya serikali yanayomtaka aondoke madarakani.

Lebanon inakabiliwa na shinikizo kutoka kwa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF kuchukua hatua za kubana matumizi ili kupata msaada wa kifedha.

((afp, dpa, Reuters))