1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Senegal yatunga sheria kali dhidi ya mapenzi ya jinsia moja

Michael Kwena
12 Machi 2026

Bunge la Senegal limepitisha muswada unaoongeza vifungo na faini kwa mahusiano ya jinsia moja. Hatua hiyo imeibua mjadala mkali, huku wakosoaji wakionya athari kwa haki za kijamii na juhudi za afya ya umma.

https://p.dw.com/p/5AIqn
Senegal Dakar 2025 | Waziri Mkuu
Bunge la Senegal likiwa kikaoni Ousmane Sonko akizungumza bungeniPicha: Papa Demba Gueye/Xinhua/picture alliance

Bunge la Senegal limeidhinisha muswada wa kisheria unaopiga marufuku mahusiano ya kingono ya watu wa jinsia moja na kuongeza kwa kiasi kikubwa adhabu kwa watakaokiuka sheria hiyo. Wabunge 135 waliunga mkono muswada huo huku watatu wakikosa kushiriki kura.

Kwa mujibu wa muswada huo, watakaopatikana na hatia ya kushiriki mahusiano ya jinsia moja watakabiliwa na kifungo cha miaka mitano hadi 10 jela, tofauti na adhabu ya sasa ya mwaka mmoja hadi mitano. Aidha, faini zinaweza kufikia takribani dola 17,700.

Sheria hiyo pia inatoa mamlaka kwa serikali kuchukua hatua dhidi ya uenezaji au ufadhili wa mahusiano ya jinsia moja, ikiwemo kupitia mashirika au vyombo vya habari. Hata hivyo, bado inahitaji kutiwa saini na rais kabla ya kuanza kutumika.

Ufaransa, Paris 2025 | Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye katika mkutano wa wajasiriamali La REF
Rais wa Senegal Bassirou Diomaye FayePicha: Federico Pestellini/PsnewZ/IMAGO

Wakosoaji waonya athari kwa haki na afya ya umma

Wakosoaji wanasema hatua hizo zinaweza kudhoofisha kazi za mashirika ya kijamii na programu za kuzuia maambukizi ya virusi vya HIV. Wakati huo huo, wafuasi wa muswada huo waliandamana jijini Dakar wakionyesha uungwaji mkono wao.

Katika ukanda wa Afrika Magharibi, mataifa mengi bado yanachukulia mahusiano ya jinsia moja kama mwiko, huku tafiti zikionyesha upinzani mkubwa wa umma. Ripoti pia zinasema watu kadhaa wamekamatwa wakihusishwa na vitendo hivyo.

Hatua ya Senegal inakuja wakati baadhi ya nchi nyingine za Afrika, zikiwemo Burkina Faso na Ghana, nazo zinajadili au tayari zimepitisha sheria zinazoongeza adhabu kwa mahusiano ya jinsia moja.

Maelfu wafurika Dakar kusherehekea ubingwa wa Senegal AFCON