Rwanda yawapa wakimbizi pasipoti | Masuala ya Jamii | DW | 11.10.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Rwanda yawapa wakimbizi pasipoti

Serikali pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la huduma kwa wakimbizi UNHCR wamesema uamuzi huo unalenga kuwapa wakimbizi uhuru wa kusafiri katika ulimwenguni bila pingamizi.

Kwa mara ya kwanza serikali ya Rwanda imeanza kutoa vibali ama pasipoti za kusafiria kwa wakimbizi wote walioko Rwanda. Serikali pamoja na shirika la umoja wa mataifa la huduma kwa wakimbizi UNHCR wote wanasema uamuzi huo unalenga kuwapa wakimbizi uhuru wa kusafiri katika nchi yoyote ulimwenguni bila kipingamizi kama ilivyokuwa awali.

Vibali hivi au pasipoti vimetengenezwa kwa njia ya ki-elektroniki na husomwa kwa kutumia kompyuta. Havina utofauti wowote na pasipoti za kawaida za mkaazi asili wa Rwanda.

Mkurugenzi mkuu wa idara ya uhamiaji nchini Anaclet Kalibata anafafanua ubora wa pasi hizi.

"Kibali hiki cha kusafiria kilitengenezwa kwa teknolojia ya kisasa kama ambayo inatumika kutengeneza pasipoti za kawaida na kinakidhi viwango vya kimataifa kuhusu uhalisia na usalama wa vibali vya kusafiria kote ulimwenguni."

Wakimbizi wameipokea habari hii kwa mikono miwili kutokana na kwamba imekuja kama suluhu la matatizo ambayo yamekuwa yakiwakumba. Frank Kaze ni mkimbizi kutoka Burundi na amekuwa nchini Rwanda kwa miaka takribani minne sasa. Anasema kwa mara mbili mfululizo alikosa fursa ya kazi nje ya Rwanda na kutokana na ukosefu wa pasi ya kusafiria kwenda hali ambayo mpaka sasa bado anakabiliana na athari zake.

Uhuru na fursa kwa wakimbizi kupanuka

Pasipoti hizo zinalenga kuwapa wakimbizi uhuru wa kusafiri katika nchi yoyote ulimwenguni bila kipingamizi kama ilivyokuwa awali.

Pasipoti hizo zinalenga kuwapa wakimbizi uhuru wa kusafiri katika nchi yoyote ulimwenguni bila kipingamizi kama ilivyokuwa awali.

Ni kutokana na changamoto kama hizi zilizomkumba Frank ambazo zimekuwa zikiwafunga wenzie kwa miaka sasa na kuwasababishia kukosa fursa muhimu. Lakini serikaliya Rwanda pamoja na shirika la umoja wa mataifa la huduma kwa wakimbizi UNHCR wote kwa kauli moja wanasema kitambulisho hiki kinanuia kupanua fursa kwa wakimbizi na kuwapa uhuru zaidi wa kutembea tofauti na kukaa kambini bila faida yoyote. Huyu ni waziri anayehusika na masuala ya wakimbizi nchini Rwanda Jean Darc de Bhoneur akiwa pamoja na mkurugenzi mkazi wa shirika la umoja wa mataifa la huduma kwa wakimbizi la UNHCR Ahmed Baba Fall.

"Wiki chache zilizopita tulitoa vitambulisho kwa wakimbizi kwa ajili ya kuwasaidia kutoka nje ya kambi na kufanya shughuli ndogondogo kwa ajili ya kujikimu lakini kuna pengine wenye uwezo wa kwenda nje ya nchi kwa ajiliya shughuli fulani, hiki kibali kitawasaidia kutoka nje ya nchi."

Waziri ameendelea kusema "kuna waliokuwa wakihitaji huduma ya matibabu baada ya kuthibitika kwamba huduma hiyo haipo hapa Rwanda, kibali hiki kitawasaidia kwenda kupata matibabu ya magonjwa sugu mataifa ya nje."

Kwa awamu ya kwanza, vimechapishwa vibali elfu 20 na kila kibali kitauzwa kwa faranga elfu sawa na dola za Marekani kumi na mbilina kitadumu kwa muda wa miaka mitano.Kibali hiki kitamruhusu mkimbizi kwenda nchi yoyote ulimwenguni isipokuwa nchi aliyoikimbia.

 

Mhariri: Saumu Yusuf

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com