1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yailaumu Ufaransa kushindwa kuzuia mauaji ya Kimbari

19 Aprili 2021

Ripoti moja iliyoandaliwa na serikali ya Rwanda inasema Ufaransa inabeba jukumu kubwa katika mauaji ya halaiki yaliyotokea nchini humo kwa kuwa ilifahamu kuwa yanaweza kutokea na hawakuyazuia.

https://p.dw.com/p/3sEmP
Ruanda Genozid
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Ripoti moja iliyoandaliwa na serikali ya Rwanda inasema Ufaransa inabeba jukumu kubwa katika mauaji ya halaiki yaliyotokea nchini humo kwani ilikuwa inafahamu huenda kukatokea mauaji kama hayo ila haikuchukua hatua zozote za kuyazuia.

Ripoti hiyo ya kurasa 600 ambayo itawekwa wazi kwa umma baadae leo baada ya kuwasilishwa mbele ya baraza la mawaziri, inasema, mbali na kutochukua hatua zozote, katika miaka 27 iliyopita Ufaransa imejaribu kuficha jukumu lake baada ya mauaji hayo ya halaiki na pia iliwapa hifadhi baadhi ya walioyachochea.

Inasema mauaji hayo yalipokuwa yanakaribia rais wa zamani wa Ufaransa Francois Mitterand na utawala wake walifahamu kuhusiana na maandalizi ya mauaji hayo ila Ufaransa ikaendelea kuiunga mkono serikali ya rais wa Rwanda wakati huo Juvenal  Habyarimana. Ufaransa ilianzisha operesheni ya kijeshi iliyopewa jina "operesheni Turquoise" iliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na iliyoanza Juni 22 ila ilikuwa imechelewa sana na haikuweza kuwaokoa Watutsi.

Frankreich, Paris: Anhörung von Felicien Kabuga zum Völkermord von Ruanda
Felicien Kabuga, miongoni mwa watuhumiwa wa mauaji hayo ya kimbariPicha: Getty Images/AFP/S. Wohlfahrt

Ripoti hiyo vilevile imesema serikali ya Ufaransa imefanya juhudi ndogo mno katika kuwafungulia mashtaka wahusika wa mauaji hayo ya halaiki kwa kuwa kufikia sasa, ni Wanyarwanda watatu tu waliofikishwa mahakamani nchini Ufaransa. Felicien Kabuga, raia wa Rwanda aliyekuwa anatafutwa kwa muda mrefu kwa kuhusika katika usambazaji wa silaha kwa wauaji, alikamatwa nje ya mji wa Paris mwezi mei mwaka jana.

Ufaransa pia imetuhumiwa vikali kwa kutoweka wazi nyaraka kuhusiana na mauaji hayo ya halaiki kwani serikali ya Rwanda iliwasilisha maombi ya nyaraka hizo mwaka 2019, 2020 na mwaka huu wa 2021 ila Ufaransa ikapuuza. Chini ya sheria za Ufaransa nyaraka zinazohusu jeshi zinaweza kuwa siri kwa miongo kadhaa ila Rais Macron mnamo Aprili 7 katika maadhimisho ya mauaji ya halaiki ya Rwanda, alitangaza uamuzi wa kuziweka wazi kwa umma kumbukumbu za mwaka 1990 hadi 1994 zinazomilikiwa na afisi ya rais wa Ufaransa na waziri mkuu.

Sikiliza hapa: 

Rwanda yawakamata watu 66 kwa kubeza mauaji ya kimbari

Ripoti hiyo inayotokana na vyanzo vya serikali kadhaa duniani, mashirika yasiyo ya kiserikali na wasomi na ambayo waandishi wake wanasema waliwahoji zaidi ya watu 250, inakuja chini ya mwezi mmoja baada ya ripoti iliyoagizwa na Rais Emmanuel Macron kusema Ufaransa "ilijitia upofu" katika maandalizi ya mauaji ya Rwanda na kisha haikuchukua hatua kwa haraka.

Ripoti hizo mbili huenda zikafungua ukurasa mpya wa mahusiano baina ya nchi hizo mbili. Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Vincent Biruta ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba nchi yake iko tayari kwa mahusiano mapya na Ufaransa. 

Mashirika: AP