Rutte asema Ulaya imepokea ujumbe wa Trump kuhusu Usalama
4 Mei 2026
Akizungumza kabla ya mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Siasa ya Ulaya (EPC) mjini Yerevan, Armenia ambao utatawaliwa na ajenda ya vita vya Ukraine na Mashariki ya Kati, Rutte alikiri kughadhabishwa kwa Marekani kutokana na hatua ya washirika wake wa Ulaya kukataa kujiunga na vita hivyo.
"Kwa ujumla, tumeona kukatishwa tamaa kwa upande wa Marekani kwa hatua za Ulaya kwa kile kinachoendelea nchini Iran na kwa Marekani kujaribu kuhakikisha kuwa dunia iko salama zaidi kwa kuhakikisha kwamba uwezo wa Iran wa nyuklia na makombora ya masafa marefu unaharibiwa. Lakini wakati huo huo, ningependa kusema, Ulaya imesikia ujumbe huo."
Rutte amesema Ulaya inajiimarisha katika kusimamia bara hilo na muungano wa NATO wakati viongozi mbali mbali wa Ulaya akiwemo Ursula von der Leyen na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa wakitilia mkazo kwamba Ulaya inapaswa kuiweka hatma mikononi mwao na kuimarisha bajeti zao za usalama na ulinzi.