1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto atetea rikodi yake licha ya maandamano ya upinzani

Admin.WagnerD
28 Machi 2023

Rais wa Kenya William Ruto ametetea rikodi yake madarakani akisema serikali anayoiongoza imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miezi sita tangu ilipochukua hatamu za uongozi.

https://p.dw.com/p/4POVv
DW-Interview mit dem Präsidenten von Kenia, William Ruto
Rais William Ruto wa Kenya akiwa kwenye mazungumzo na Shirika la Utangazaji la DW.Picha: Zura Karaulashvili/DW

Rais Ruto aliye ziarani barani Ulaya ametoa matamshi hayo wakati wa mahojiano maalumu la shirika la utangazaji la DW ambapo amegusia masuala chungunzima ikiwemo hali ya maisha nchini Kenya, mikakati yake ya kutimiza ahadi za uchaguzi na vurumai inayotokana na maandamano ya upinzani dhidi ya utawala wake.

Kwenye mahojiano hayo yaliyofanyika mjini Berlin, Ruto amejinasibu kuwa serikali yake imefanikiwa kuirejesha Kenya kwenye mkondo unaofaa kiuchumi na kuimarisha hali ya usalama. 

Amesema katika kipindi tangu alipoapishwa mwaka uliopita, ameshughulikia kwa umakini suala la kupanda kwa gharama za maisha ambalo limekuwa mwiba mchungu kwa utawala wake. 

Kiongozi huyo ambaye yuko nchini Ujerumani tangu siku ya Jumatatu kwa mazungumzo na viongozi wakuu mjini Berlin, ameikingia kifua mipango ya serikali yake ya kushughulikia kupanda kwa gharama za maisha ikiwemo uagizaji wa shehena ya chakula kutoka nje ili kupunguza makali ya bei .

"Hivi sasa tunawekeza kwenye umwagiliaji na hiyo ni sehemu ya kile nitakachojadili na maafisa wa Ujerumani juu ya jinsi tunavyoweza kukibadili kilimo cha Kenya kutoka kutegemea mvua na kuwa cha umwagiliaji. Kwa hivyo mpango wa muda mfupi ni kuagiza (chakula) kutoka nje, kwa muda wa kati ni kuwasaidia wakulima na kwa muda muda mrefu ni umwagiliaji” amesema rais Ruto.

Ruto: Maandamano ya upinzani hayana uhusiano na ughali wa maisha 

Hata hivyo suala la gharama za maisha na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu limesadifu kuwa kihunzi kirefu kwa utawala wake. Upinzani ukiongozwa na mwanasiasa wa siku nyingi Raila Odinga ulifanya duru nyingine ya maandamano makubwa siku ya Jumatatu kuongeza shinikizo kwa utawala wa Ruto kushughulikia hali ngumu ya maisha. 

Kenia | Anti-Ruto-Proteste in Kisumu
Picha: Musa Naviye/DW

Kwenye mahojiano na DW, rais Ruto amewakosoa wapinzani wake kwa kufanya kile amekiita "vurugu” ambazo anasema hazina uhusiano na kupanda kwa gharama za maisha nchini Kenya.

"Vurugu mjini Nairobi hazina uhusiano sana na kupanda kwa gharama za maisha. Bali zinahusiana na baadhi ya matokeo ya uchaguzi, suala ambalo limeshafungwa muda mrefu. Lakini kwa kuwa gharama za maisha ni suala linalovutia hisia za watu, washindani wetu wanajaribu kulitumia hilo. Hata hivyo ni hakika Wakenya ni watu werevu sana.” amekaririwa akisema rais Ruto.

Akizungumzia uwezekano wa kufanya mazungumzo na upinzani ili kumaliza wimbi la maandamano, Ruto amesema yuko tayari kushirikiana na makundi yote nchini Kenya lakini amesisitiza mazungumzo yoyote yatakayofanyika hayatagusia uhalali wa uchaguzi uliomwingiza madarakani mwaka uliopita.

"Upinzani unataka majadiliano kuhusu uchaguzi ulifanyika miezi sita iliyopita, uchaguzi ambao ulishuhudiwa na Jumuiya ya Kimataifa, uchaguzi uliosifiwa na Umoja wa Ulaya. Wanataka tufanye mazungumzo kuhusu hilo. Mazungumzo ya aina hiyo yako nje ya katiba” amesisitiza kiongozi huyo. 

Wito wa kushughulikia Mabadiliko ya Tabianchi watolewa 

Berlin | Bundespräsident Frank Walter Steinmeier trifft mit Kenias Präsident William Ruto
Rais William Ruto wa Kenya akikagua gwaride la heshima kwenye ofisi ya rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier mjini Berlin.Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Kwenye mahojiano hayo, Ruto pia amesifu mageuzi aliyoyafanya katika mfumo wa utoaji haki nchini Kenya na kupuuza ukosoaji kuwa chini ya utawala wake kesi za ufisiadi na rushwa zimeondolewa mahakamani kwa kile kinachoelezwa kuwa shinikizo kutoka ngazi ya juu.

Mbali ya masuala ya ndani ya Kenya rais Ruto amegusia vilevile haja ya kumalizwa mzozo kati ya Urusi na Ukraine pamoja na mizozo kwenye maeneo mengine duniani.

Kadhalika ametoa rai kwa mataifa tajiri kuzisaidia nchi masikini kupambana na mabadiliko ya tabianchi akisema nchi zisizo na nguvu kiuchumi ndiyo zinalipa gharama kubwa kutokana na athari za kuongezeka kwa joto kwenye uso wa dunia.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi