Rasi ya Korea: Hatma ya Kaesong mashakani | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.04.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rasi ya Korea: Hatma ya Kaesong mashakani

Wafanyakazi wa Korea Kusini wanajiandaa kuondoka kutoka eneo la viwanda la Kaesong leo Jumamosi (27.04.2013), kufuatia hatua ya utawala wa mjini Seoul kutangaza kujitoa kabisaa katika mradi huo wa pamoja.

Muonekano jumla wa eneo la viwanda la Kaesong.

Muonekano jumla wa eneo la viwanda la Kaesong.

Hatua hii inauweka mashakani mustakabali wa eneo la Kaesong, ambalo hapo awali lilikuwa ishara ya ushirikiano katika mpaka baina ya nchi hizo mbili, ambao unasemekana kuwa ndiyo wenye shughuli nyingi zaidi za kijeshi duniani, na chanzo muhimu cha fedha taslimu kwa utawala uliyotengwa wa Kim Jong-Un nchini Korea Kaskazini.

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Un.

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Un.

Korea Kusini iliyokatishwa tamaa, ilisema siku ya Ijumaa kuwa imeamua kuondoa wafanyakazi wake 175 waliosalia katika eneo hilo, baada ya Pyongyang kukataa kushiriki mazungumzo rasmi ya kuanzisha tena shughuli katika eneo hilo, katika muda wa mwisho ulioyotolewa na Kusini. "Serikali imechukua hatua isiyoepukika ya kuondoa watu wote waliosalia kwa usalama wao," alisema waziri wa muungano wa Kusini, Ryoo Kihl-Jae.

Wamiliki wahofia kupoteza vitega uchumi vyao

Kampuni za Korea Kusini zilizo na viwanda katika eneo hilo zimeelezea kushtushwa, huku baadhi zikitishia kupuuza agizo la kuondoa wafanyakazi, katika jitihada za kulinda uwekezaji wao. Msemaji wa wizara ya muungano alisema wafanyakazi 127 walitarajiwa kuvuka mpaka kurudi Kusini katika misafara miwili ya magari siku ya Jumamosi mchana. Watu 48 waliobakia, wengi wao wakiwa wafanyakazi wa serikali wanaoendesha eneo hilo la viwanda, na wahandisi wa simu na umeme, wataondolewa siku ya Jumatatu, kwa mujibu wa msemaji huyo.

Lakini mfanyabiashara moja mwenye maslahi katika eneo la Kaesong alisema nyingi ya kampuni 123 za Korea Kusini zinazoendesha shughuli zao katika eneo hilo zilikuwa zinapinga hatua hiyo."Baadhi wanasema tukubaliane na ombi la serikali kuondoka eneo hilo, lakini wengine wengi hawataki kuondoka kwa khofu ya kupoteza vitega uchumi vyao," aliiambia AFP akiomba jina lake lihifadhiwe.

Mfanyabiashara huyo aliongeza kuwa pia wafanyakazi wengi waliobakia Kaesong wanasita kuondoka kwa sababu wanahisi watapata tabu kupata kazi nyingine, na kusema kuwa wafanyakazi hao bado wana chakula cha kutosha. Eneo hilo limeathirika kutoka na kuongezeka kwa wasiwasi kulikosababishwa na jaribio la nyuklia la Korea Kaskazini mwezi Februari, ambalo lilikuja baada ya mwaka mmoja tangu Kim Jong-Um kuchukua madaraka, kufuatia kifo cha baba yake Kim Jong-il.

Wanawake kutoka Korea Kaskazini wakifanya kazi katika kiwanda cha nguo cha Korea Kusini kilichopo eneo la Kaesong.

Wanawake kutoka Korea Kaskazini wakifanya kazi katika kiwanda cha nguo cha Korea Kusini kilichopo eneo la Kaesong.

Pyongyang ambayo imetaka kukomeshwa kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa na kusimamishwa kwa mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Marekani na Kusini, iliamua tarehe 3 April, kuizuia Kusini kuingia katika eneo la Kaesong, inagawa iliwaruhusu wafanyakazi kuondoka. Siku chache baadaye, Korea Kaskazini iliondoa wafanyakazi wake wote 53,000 na kusimamisha shughuli zote, ikikasirishwa na hatua ya Kusini kuzungumzia mpango wa kijeshi kulinda wafanyakazi wake walioko eneo hilo.

Kinachofuata baada ya hapo

Yang Moo-Jin, Profesa katika chuo kikuu cha masuala ya Korea Kaskazini kilichopo mjini Seoul alisema hatua itakayofuata ya Korea Kusini ni kukata umeme katika eneo hilo kabla ya kulifunga kabisaa. Alisema mwitikio imara wa Korea Kusini unaweza kusababisha kutoweka kabisaa kwa kituo kilichosalia cha mawasiliano-- na makabiliano ya muda mrefu--kati ya Korea mbili.

Kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 2004, kiko umbali wa kilomita 10 ndani ya Korea Kaskazini, ambayo kimsingi bado iko katika vita na Kusini, baada ya vita vya Korea vya mwaka 1950-53 kumalizika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, badala ya mkataba wa amani. Seoul imeitaka Kaskazini kuhakikisha wafanyakazi wake wanarejea salama, na kulinda mali za kampuni zilizoko Kaesong.

Dereva wa gari wa Korea Kusini akiulizwa maswali na waandishi wa habarim baada ya kurejea kutoka eneo la Kaesong. Waandishi walizuiwa pia kuingia eneo hilo.

Dereva wa gari wa Korea Kusini akiulizwa maswali na waandishi wa habarim baada ya kurejea kutoka eneo la Kaesong. Waandishi walizuiwa pia kuingia eneo hilo.

Ikikataa pendekezo la majadiliano, Kamisheni ya taifa ya ulinzi ya Kaskazini ilionya siku ya Ijumaa, kwamba eneo la Kaesong hivi sasa liko katika ukingo wa kuporomoka. Katika taarifa yake, Kamisheni hiyo ililaumu kile ilichokiita mpagao wa kizembe wa kivita kutoka utawala kibaraka wa Kusini.

Mradi wa Kaensong ulianzishwa chini ya sera ya "Sunshine" ya maridhiano baina ya Korea mbili mwishoni mwa miaka ya 1990, na rais wa Korea Kusini wakati huo, Kim Dae-Jung. Linaendeshwa kama kanda ya pamoja ya ushirikiano wa kimaendeleo, likiwa na kampuni za Korea Kusini zinazovutiwa na vyanzo vyake vya nguvu kazi rahisi, iliyo elimika na yenye ujuzi, likiripotiwa kuingiza dola 469.5 milioni katika mwaka wa 2012.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe.
Mhariri: Amina Abubakar

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com