1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChad

Rais wa mpito wa Chad Deby aanza kampeni za uchaguzi wa Mei

Bruce Amani
15 Aprili 2024

Rais wa mpito wa Chad Mahamat Idriss Deby ameanza rasmi kampeni yake ya uchaguzi wa mwezi Mei unaopaswa kumaliza utawala wa kijeshi uliodumu kwa miaka mitatu akiahidi kuimarisha usalama na kuukuza uchumi.

https://p.dw.com/p/4ekoy
Rais wa mpito wa Chad Deby
Rais wa mpito wa Chad Deby anatazamiwa kushinda uchaguzi wa Mei baada ya wapinzani kufungiwa kugombeaPicha: Denis Sassou Gueipeur/AFP/Getty Images

Serikali ya Deby ni moja ya tawala za kijeshi zilizokamata madaraka Afrika magharibi na Kati tangu mwaka wa 2020, na kuzusha wasiwasi wa kurudi nyuma demokrasia.

Chad ndio ya kwanza kati ya tawala hizo kuandaa uchaguzi licha ya shinikizo la kikanda na kimataifa la kutaka madaraka yarejeshwe mara moja kwa raia. Deby aliuambia umati mkubwa wa watu katika mji mkuu N'Djamena kuwa sasa wapo katika kona ya mwisho ya barabara ya kureja kwa utawala wa kikatiba. Mwezi uliopita, wagombea 10 wakiwemo wapinzani wawili wakali wa utawala wa kijeshi walifungiwa kugombea katika uchaguzi huo. Ni mpinzani wa zamani Succes Masra pekee, ambaye sasa ni waziri mkuu, aliyesalia kinyang'anyironi.

Soma pia: Mamilioni ya watu wanakabiliwa na kitisho cha ukosefu wa chakula Chad

Jenerali Deby mwenye umri wa miaka 40 alitwaa madaraka katika mwaka wa 2021 wakati baba yake aliyetawala kwa muda mrefu Idriss Deby alipouawa kwenye uwanja wa vita dhidi ya waasi kaskazini mwa nchi hiyo. Awali aliahidi kurejesha utawala wa kiraia katika miezi 18.

Lakini serikali yake ikasogeza mbele hadi mwaka wa 2024 na kumruhusu kugombea urais. Kucheleweshwa kwa uchaguzi kulizusha maandamano yenye ghasia yaliyovunjwa na vikosi vya usalama na kusababisha vifo vya karibu raia 50.