1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu wa Chad atangaza kuwania urais

Bruce Amani
11 Machi 2024

Waziri mkuu aliyeteuliwa na serikali ya kijeshi Chad ametangaza kuwa atashiriki uchaguzi wa rais wa Mei 6, siku chache tu baada ya kiongozi aliyeko madarakani Jenerali Mahamat Idriss Deby Itno kutangaza kuwania urais.

https://p.dw.com/p/4dNxo
Waziri Mkuu wa Chad Succes Masra na Waziri Mkuu wa Ufaransa Gabriel Attal
Waziri Mkuu wa Chad, Succes Masra (kushoto), akiwa na mwenzake wa Ufaransa, Gabriel Attal.Picha: Lafargue Raphael/abaca/picture alliance

Succes Masra, kiongozi wa zamani wa upinzani, alirejea kutoka uhamishoni na kutia saini mkataba wa maridhiano na Deby Itno kabla ya kuwa waziri mkuu mwaka huu.

Upinzani unasema kuwa hatua ya Masra kugombea ni njama ya kutoa sura ya kuwepo vyama vingi katika uchaguzi huo ambao kiongozi huyo wa kijeshi ana uhakika wa kushinda huku wapinzani wake wakuu wakiwa ama wameuawa au kukimbilia uhamishoni.

Soma zaidi: Kiongozi wa kijeshi wa Chad atangaza kuwania uchaguzi wa rais wa mei 6

Masra, mwenye umri wa miaka 40, alitangaza azma yake ya kuwania urais katika mkutano wa kampeni uliohudhuriwa na mamia ya wafuasí wa chama chake cha Transformers yaani wapenda mabadiliko, akisema anataka "kuponya mioyo na kuwaunganisha watu".