Rais wa FIFA Sepp Blatter akata rufaa kupinga kusimamwishwa | Michezo | DW | 09.10.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Rais wa FIFA Sepp Blatter akata rufaa kupinga kusimamwishwa

Rais wa shirikisho la kandanda ulimwenguni FIFA Sepp Blatter amekata rufaa dhidi ya uamuzi uliochukuliwa na shirikisho hilo wa kumfungia siku 90 kutojihusha na masuala yoyote yanayohusu kandanda.

Rais wa FIFA Sepp Blatter.

Rais wa FIFA Sepp Blatter.

Kwa mujibu wa mwanasheria wa Blatter, kutoka nchini Marekani Richard Cullen rufaa hiyo tayari imewasilishwa katika kamati ya rufaa ya FIFA.

Mwanasheria huyo alisema anatarajia kuwasilisha ushahidi utakaothibitisha ya kwamba mteja wake hausiki na tuhuma hizo.

Hatua hii inakuja mnamo wakati mshauri wa Rais huyo wa FIFA, Klaus Stoehlker akisema rufaa hiyo haitakuwa na maana yoyote ile.

Kamati ya maadili ya shirikisho hilo hapo jana ilitoa uamuzi wa kumfungia Sepp Blatter pamoja na Rais wa shirikisho la kandanda barani Ulaya Michel Platini kwa muda wa siku tisini kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa fedha ndani ya shirikisho hilo ambapo inadaiwa kuwa mnufaikaji wa malipo hayo yanayodaiwa kutokuwa halali ni Michel Platini.

Mwanasheria mkuu wa serikali ya Uswisi alisema ya kuwa Septemba 25 mwaka huu idara yake ilikuwa tayari imeanzisha uchunguzi dhidi ya Blatter kuhusiana na malipo ya kiasi cha fedha zipatazo milioni 2, kwa thamani ya fedha za Uswisi mnamo mwaka 2011 kwenda katika akaunti ya Platini na pia kuhusiana na sakata la mikataba ya haki za matangazo ya televisheni za Caribbean.

Blatter adai tuhuma hizo hazina ukweli

Hata hivyo Blatter raia wa Uswisi ambaye amekuwa kiongozi wa shirikisho hilo la kanadanda ulimwenguni tangu mwaka 1998 alilieleza gazeti moja nchini Ujerumani wiki hii ya kuwa hatua ya uchunguzi huo dhidi yake si sahihi.

Hivi sasa viongozi hao wawili wanachunguzwa na mamalaka za serikali ya uswisi.

Platini kama ilivyo kwa upande wake Blatter amesema naye pia atakata rufaa kupinga hukumu hiyo na kusema kuwa hausiki hata kidogo na tuhuma hizo.

Viongozi hao wa soka watatumikia adhabu hiyo katika kipindi cha siku hizo tisini kama haita futwa ingawa pia inaweza kuongezwa kwa siku nyingine 45.

Platini ni mmoja wa wale wanaowania nafasi ya urais wa FIFA katika uchaguzi mwingine uliotishwa mwezi Februari mwakani ingawa pia kabla ya kupitishwa kwake itabidi ahojiwe juu ya uadilifu wake.

Kiongozi mwingine ambaye pia anawania nafasi hiyo nzito ndani ya shirikisho hilo ni Chung Mong Joon kutoka Korea kusini ambaye alifungiwa hapo jana miaka sita kwa tuhuma za masuala mengine yanayohusu shirikisho hilo.

Kwa mujibu wa taratibu za FIFA Makamu wa Rais mwandamizi wa FIFA kutoka nchini Cameroon Issa Hayatou ndiyo kwa sasa anakaimu nafasi hiyo ya Rais wa FIFA.

Mwandishi: Isaac Gamba/DPAE/ECA

Mhariri :Yusuf Saumu