Rais Obama atatembelea Kogelo? | Matukio ya Afrika | DW | 20.07.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Rais Obama atatembelea Kogelo?

Bado hakuna uhakika iwapo Barack Obama atatembelea Kogelo, kijiji cha ndugu zake, atakapokuwa ziarani Kenya. Hata hivyo wakazi wanajiandaa kwa ujio wa kushtukiza wa Obama, wanayemchukulia kama mwanao.

Siku chache tu kabla ya Raisi wa Marekani Barack Obama kuwasili nchini Kenya kwa kongamano la dunia la ujasiriamali, haijabainika kama atazuru jamaa yake nchini Kenya katika kijiji cha Nyan’goma Kogelo, kilicho katika Kaunti ya Siaya, kilomita chache kutoka mji wa Kisumu.

Hofu ya Obama kutotembelea eneo hili ambapo pia ndipo alipozikwa babake imeanza kudhihirika, kutokana na wito wa jamaa yake kwa wakazi wa Kogelo kuwa Obama ni kiongozi aliye na shughuli nyingi anayefaa kueleweka hata asipofika hapa.

Kauli kama hii ilitolewa pia na Balozi wa Marekani nchini Kenya Robert, jambo ambalo limeonekana kuwavunja moyo wakazi wa eneo hili la Kisumu na Kogelo.

Wengine hata hivyo wanajipa moyo kwamba kutobainika wazi kuhusu ziara yake hapa inatokana na sababu za kiusalama na kwamba huenda akafika hapa bila ya kutarajiwa au kisirisiri.

Bibi Sarah Obama ajiandaa kumpokea mjukuu

Sarah Obama, bibi yake Barack Obama

Sarah Obama, bibi yake Barack Obama

Serikali ya Kaunti ya Siaya kwa kuhofia kwamba huenda Raisi Obama asiitembelee jamaa yake katika kijiji cha Nyan’goma Kogelo katika kaunti hii, imetenga shilingi karibu milioni 50 zitakazotumika kwa tafrija mbali mbali wakati wa ziara yake hapa, na hata kumjengea Bibi yake Obama, Sarah Obama, chumba kidogo cha kupokelea wageni.

Hofu ya kutozuru ilianza kudhihirika wakati jamaa ya Obama kijijini Kogelo, kupitia kwa msemaji wao Masat Obama ambaye ni dada wa kambo wa Rais Obama, ilipowaambia waandishi wa habari kwamba hawana hakika ya kuja kwake kijijini, na kwamba kama mtoto wa nyumbani yuko huru kufika wakati wowote bila ya kutoa taarifa.

Wafanyabiashara wengi ambao wamekuwa wakiuza bidhaa mbali mbali, kama vile fulana na kofia zilizo na picha za Rais huyu, pamoja na bendera za Marekani na Kenya tangu safari hii ya Obama Kenya ilipotangazwa, wameonyesha pia masikitiko yao.

Kogelo yapata miundombinu mipya

Licha ya sintofahamu hii, usalama katika boma la Mama Sarah kama anavyojulikana bibi yake Raisi Obama umeimarishwa zaidi wakati huu, kama anavyoelezea Bi Caroline Onchoka Kamishna wa Siaya ambaye pia anayesimamia usalama. “Tunaendelea na doria kama kawida, Tumegundua kuwa mji huu unapokea wageni wengi, na tuko hapa kuimarisha usalama, kwa enzi hii ya Al Shabaab huwezi kujua linaloweza kutokea. Na tunataka kuwa tayari kwa lolote wakati wowote.”

Tangu achaguliwe kuwa Seneta na baadaye Rais wa Marekani, kijiji kidogo cha Kogelo kilichokua kimelala kimepata miundombinu bora kama vile barabara, umeme, maji na shule pamoja na hoteli za kitalii.

Rais Barack Obama anatarajiwa nchini Ijumaa ambapo ataongoza kongamano la kimataifa la ujasiriamali pamoja na Raisi Uhuru Kenyatta wa Kenya. Kongamano hili linatarajiwa kuhudhuriwa na wakuu wa mashirika mbali mbali, asasi za kijamii, na wajasiriamali zaidi ya 3000 wanaohimizwa kuwekeza hapa Afrika.