1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais na bunge waingia kwenye mvutano wa wazi Iran

Saumu Mwasimba
2 Desemba 2020

Rais Rouhani aukataa muswaada wa sheria uliopitishwa na bunge utakaozuia Umoja wa Mataifa kuingia Iran kufanya shughuli zozote za ukaguzi wa Nyuklia. Bunge linasema nguvu za Nyuklia za Iran haziwezi kuzuiwa

https://p.dw.com/p/3m6eK
 Hassan Rouhani Präsident Iran
Picha: Alexei Druzhinin/Sputnik/AFP

Hassan Rouhani ameukataa muswada huo akisema ni muswaada wenye madhara katika  juhudi za kidiplomasia zinazolenga kuyapa tena uhai au kuyarudisha makubaliano ya kimataifa ya Nyuklia yaliyofikiwa mwaka 2015 na hatimaye kulegezwa vikwazo vya Marekani. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Saeed Khatibzadeh,amefafanua zaidi msimamo huu wa Rouhani kwa kusema.

''Tangazo la serikali limeweka wazi kwamba haikubaliani na mpango huu. Serikali imesema kwamba mpango huu hauhitajiki na wala hauna maana''

Mvutano kuhusu muswaada huo wa Nyuklia  uliopata nguvu zaidi baada ya kuuwawa kwa mwanasayansi wa jamhuri hiyo ya kiislamu unaonesha kuwepo uhasama kati ya rais Rouhani mwenye msimamo wa wastani na wabunge wenye msimamo mkali waliohodhi bunge la nchi hiyo na wanaopendelea zaidi mwelekeo  wa mapambano dhidi ya nchi za Magharibi.

Iran Parlament
Picha: Iranian Presidency/ZUMA Wire/picture alliance

Rais Rouhani anasema wabunge wanatumia muswaada huu kujiweka katika nafasi nzuri kuelekea uchaguzi ujao wa Juni 2021 lakini serikali yake inautazama kama muswada usiokuwa na faida yoyote katika mkondo wa kidiplomasia.

Lakini pia msemaji wa serikali Ali Rabiei amesema bunge halina mamlaka ya kushughulikia masuala ya sera za Nyuklia kwa namna yoyote ile, ni baraza la usalama tu la nchi hiyo ndilo lenye jukumu hilo. Shirika la nguvu za Atomiki la Iran AEOI pamoja na wizara ya mambo ya nje pia wameukosoa muswaada huo wa sheria kwa kusema hauna mantiki kisiasa na hauzingatii hali halisi. Kwa maneno mengine muswaada huu umezusha mvutano wa wazi kabisa nchini Iran.

Kimsingi mswaada huu unaozungumziwa ni muswaada ambao kwa hakika ungezuia Umoja wa Mataifa kufanya shughuli yoyote ya ukaguzi ndani ya Iran na pia ungeipa nafasi serikali kuanzisha tena shughuli ya kurutubisha madini ya urani kwa asilimia 20 endapo nchi za Ulaya zitashindwa kuipa jamhuri hiyo ya kiislamu msaada kutokana na vikwazo vya Marekani vilivyowekwa dhidi ya sekta za mafuta na benki za nchi hiyo.

Iran | Ali Khamener tifft Mitgliedern des Nationalen Anti-Corona-Stab
Picha: khamenei.ir/MEHR

Kiwango hicho cha asilimia 20 cha urutubishaji Urani bado hakijafikia kiwango kinachohitajika kwa ajili ya kutengeneza silaha za Nyuklia lakini ni kiwango kikubwa kuliko kile kinachotakiwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya shughuli za kiraia. Lakini juu ya yote kiongozi wa juu kabisa Ayatollah Ali Khamenei ndiye mwenye kauli ya mwisho katika sera zote muhimu za nchi ikiwemo zile zinazohusiana na mpango wa Nyuklia.

Ama kuhusu suala la Iran rais mteule wa Marekani ametowa msimamo wake na kusema serikali yake itaondowa vikwazo dhidi ya Iran ikiwa serikali ya mjini Tehran itarudi kwenye makubaliano ya Nyuklia.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Josephat Charo