Rais Kabila, Museveni na Kagame watoa tamko juu ya mgogoro wa Kongo | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.11.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais Kabila, Museveni na Kagame watoa tamko juu ya mgogoro wa Kongo

Viongozi wa Uganda, Kongo na Rwanda kwa pamoja wamewataka waasi wa M23 katika jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo ambao wamekuwa wakisonga mbele baada ya kuuteka mji wa Goma, kurudi nyuma na kuuachia mji huo.

Marais Paul Kagame, Yoweri Museveni na Joseph Kabila

Marais Paul Kagame, Yoweri Museveni na Joseph Kabila

Kulingana na msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Uganda, rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni, Paul Kagame wa Rwanda na rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya kongo Joseph Kabila wamelitaka kundi la waasi la M23 kutoka mjini Goma mara moja.

Akizungumza na shirika la habari la dpa, msemaji huyo James Mugume, amesema waasi hao wametakiwa kurudi katika meza ya mazungumzo badala ya kuendeleza mgogoro. Viongozi hao walikutana mjini Kampala.

Baadhi ya raia wa Kongo wakikimbilia usalama wao

Baadhi ya raia wa Kongo wakikimbilia usalama wao

Kwa upande wao mawaziri wa mambo ya nchi za nje kutoka nchi tisa za Afrika, ambao wamekuwa wakikutana nchini Uganda kuijadili hali nchini Kongo wameitaka jamii ya kimataifa kutoa msaada wa kidiplomasia na kibinaadamu katika kutafuta suluhu ya mgogoro wa Kongo.

Mawaziri hao pia wamelitaka baraza la usalama la Umoja wa Afrika kutoa agizo kwa kikosi chake cha Kimataifa huku wakitafuta uungaji mkono wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kutuma jeshi hilo Mashariki mwa Kongo.

Marekani nayo imewataka waasi kuondoka mjini Goma na kuachana na mipango ya kuteka miji mingine. Marekani pia imesema inalaani msaada wowote kutoka nje kwa waasi hao.

Waasi wakataa Ombi

Waasi wa M23

Waasi wa M23

Huku hayo yakiarifiwa waasi wa M23 wanaendelea kusonga mbele, baada ya kuuteka mji wa Goma sasa wameudhibiti pia mji wa Sake. Waasi hao wanaendelea na mpango wao wa kutaka kuiteka miji ya Bukavu, Kisiangani na Kinshasa.

Askofu Jean-Marie Runiga mkuu wa kundi hilo la M23 amesema hawatatoka mjini Goma, kama walivyoombwa na viongozi hao na kwamba watasonga mbele zaidi hadi pale rais Joseph Kabila atakapokutana nao kwa mazungumzo. Runiga amesema hana imani kwamba rais Kabila kweli anataka mazungumzo nao na kwamba wataendelea kukaa Goma hata wakishambuliwa wako tayari kujilinda na kusonga mbele.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Mapema jana wajumbe wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walifanya mkutano wa dharura mjini New York Marekani na kwa pamoja wakapitisha azimio kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, baada ya waasi kuteka mji wa Goma. Azimio hilo limetowa wito wa kusitishwa mapigano mara moja.

Wakati huo huo ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema kamanda mkuu wa jeshi la la nchi kavu la Kongo anasemekana amekuwa akiwauzia silaha waasi nchini humo. Ripoti hiyo inasema kuwa Generali Gabriel Amisi amekuwa akiongoza mtandao wa kuwauzia silahawaasi. Hata hivyo waasi wa M23 waliouteka mji wa Goma si miongoni mwa waasi waliopokea silaha hizo.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Sauti na Vidio Kuhusu Mada

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com