1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raila Odinga amesema muungano wa NASA umesambaratika

10 Agosti 2020

Kiongozi wa chama cha Upinzani cha ODM nchini Kenya Raila Odinga amekiri kuwa Muungano Mkuu wa Upinzani nchini humo, NASA umesambaratika.

https://p.dw.com/p/3giH2
Kenia Oppositionsführer Musalia Mudavadi, Raila Odinga, Isaac Ruto, Kalonzo Musyoka, and Moses Wetangula  in Nairobi
Picha: Reuters/T. Mukoya

Raila Odinga amedai kuwa miungano hufa isiposhinda kwenye uchaguzi na hivyo ndivyo muungano huo ulivyosambaratika baada ya uchaguzi mkuu uliopita. Hata hivyo kiongozi mwenza kwenye muungano huo Musalia Mudavadi ametofautiana na kauli ya Raila.

Nyufa kwenye Muungano Mkuu wa upinzani NASA, zilianza kudhihirika pindi tu, kiongozi wake Raila Odinga alipozika tofauti zake za kisiasa na rais Uhuru Kenyatta, katika kile kilichokuja kufahamika kuwa salamu za heri, baada ya uchaguzi wenye utata mwaka 2017. Baadaye kiongozi mwenza wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka alipewa wadhifa wa kuwa mjumbe maalum kwenye mzozo wa Sudan Kusini na hata akasaini mkataba wa ushirikiano na chama tawala cha Jubilee.

Huu ni msumari wa mwisho kwa muungano wa NASA

Kenia Raila Odinga bei Kundgebung in Mombasa
Kiongozi wa chama cha siasa cha ODM Raila OdingaPicha: Reuters/J. Okanga

Msumari wa mwisho umegongelewa kwenye jeneza la muungano huo baada ya matamshi ya Raila kuwa kipindi cha muungano huo kimekamilika. Kauli ya Raila inatia kikomo mahusiano ya kisiasa ambayo amekuwa nayo na viongozi wenza wa Muungano huo kama vile Musalia Mudavadi wa chama cha Amani National Congress na Moses Wetangula wa Ford Kenya. Viongozi hao walimuunga mkono Raila kwenye uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2017. 

Matamshi ya kiongozi wa ODM yanajiri huku wito wa kuwa na mwaniaji mmoja kwenye kiti cha urais ukiongezeka. Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyikazi nchini Francis Atwoli akimuidhinisha Raila kuwa anayefaa kuongoza taifa hili kwenye uchaguzi mkuu ujao. Raila mwenyewe amekataa kugusia azma yake kwenye uchaguzi ujao.

Soma zaidi:Raila Odinga ataka "Punguza Mizigo" ikataliwe

Hata hivyo ni kauli ya Katibu Mkuu, wa chama cha Jubilee David Murathe aliyesema kuwa Raila atakuwa rais kwenye uchaguzi mkuu ujao, kwa kila hali, inayozidi kuwashangaza wakenya. Murathe ni mshirika wa karibu wa rais Kenyatta.

Chanzo: DW