1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUrusi

Putin atishia kushambulia Magharibi kupitia mataifa mengine

6 Juni 2024

Rais Valdimir Putin ameonya jana Jumatano kwamba Urusi inaweza ikawapatia mataifa mengine makombora ya masafa marefu kwa ajili ya kushambulia maeneo lengwa kwenye mataifa ya magharibi.

https://p.dw.com/p/4ght8
Rais Vladimir Putin wa Urusi I Uzbekistan
Rais wa Urusi Vladimir Putin ameonya kuyashambulia mataifa ya magharibi kupitia mataifa mengine baada ya kuiruhusu Ukraine kutumia silaha zake kuwashambuliaPicha: Mikhail Metzel/REUTERS

Hatua hii amesema itakuwa ni jibu ya ruhusa iliyotolewa na washirika wa jumuiya ya NATO kwa Ukraine kutumia silaha inazopewa na magharibi kuishambulia Urusi.

Putin aidha amethibitisha kwa mara nyingine kuhusu utayari wa kutumia silaha za nyuklia ikiwa kutakuwa na kitisho chochote kwenye eneo lake.

Soma Pia: Putin aonya juu ya kuwepo wanajeshi wa Ufaransa huko Ukraine

Amesema hatua hiyo ya magharibi itazidi kudhoofisha usalama wa kimataifa na kuchochea matatizo makubwa, na kuashiria wazi ushiriki wake wa moja kwa moja kwenye vita kati ya Urusi na Ukraine na kuongeza kuwa wana haki ya kuchukua hatua kama hiyo.

Putin alikuwa akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo vya magharibi, jambo ambalo analifanya kwa nadra mno tangu alipoivamia Ukraine.

Marekani na Ujerumanihivi karibuni waliiruhusu Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu waliyoipatia kushambulia baadhi ya maeneo ndani ya Urusi.

Singapore | Mkutano wa kilele wa 21, Shangri-La- | Volodymyr Zelenskyy
Rais Volodymyr Zelensky akiwa kwenye kongamano la kilele la usalama la 21 la Shangri-La huko Singapore ambako alihimiza mataifa kumuunga mkono katika vita dhidi ya UrusiPicha: Nhac Nguyen/AFP/Getty Images

Siku ya Jumatano, afisa mmoja wa magharibi pamoja na seneta wa Marekani walisema Ukraine imetumia silaha walizopewa na taifa hilo kushambulia ndani ya Urusi chini ya idhini hiyo inayosimamiwa na Rais Joe Biden, ambapo Ukraine watatumia silaha hizo, lakini kwa masharti, katika kuupigania mji wake wa Kharkiv.

Soma pia: Ukraine kuomba idhini pana ya kushambulia ndani ya Urusi

Putin asisitiza kwamba Urusi haikuanzisha vita nchini Ukraine

"Kama mtu anadhani inawezekana kupeleka silaha kwenye uwanja wa vita ili kushambulia eneo letu na kutuletea matatizo, kwa nini na sisi hatuna haki ya kupeleka silaha kama hizo kwenye maeneo mengine duniani ambako wanaweza kushambulia maeneo muhimu kwenye mataifa ya magharibi?" alihoji Putin.

"Hilo litakuwa jibu linalowiana. Tutafikiria kuhusu hilo," aliwaambia waandishi hao wa habari, huku akipuuzilia mbali madai kwamba Urusi inapanga kuwashambulia wanachama wa NATO.

Putin, ametumia pia fursa hiyo kurudia na kusisitiza kwamba nchi yake haikuanzisha vita dhidi ya Ukraine, na badala yake alipeleka lawama zake kwenye vuguvugu lililoanza mnamo mwaka 2014 la wanaounga mkono mataifa ya magharibi

"Kila mmoja anadhani Urusi ilianzisha vita nchini Ukraine. Ningependa kusisitiza kwamba si Magharibi wala Ulaya anayetaka kukumbuka namna janga hili lilivyoanza," alisema Putin.   

Hata hivyo, Putin alikataa kutaja idadi ya wanajeshi waliokufa kwenye vita hivyo vya miaka miwili, akisema tu kwamba idadi ya vifo vya wanajeshi wa Ukraine imezidi mara tano ya wale wa Urusi.