1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroNepal

Polisi Nepal: Vifo kufuatia maandamano vimeongezeka

12 Septemba 2025

Polisi Nepal imesema idadi ya vifo imeongezeka kutokana na maandamano ya wiki hii huku Rais wa nchi hiyo na mkuu wa majeshi wakitarajiwa kufanya mkutano muhimu hii leo ambapo majina ya viongozi wa mpito yatapendekezwa.

https://p.dw.com/p/50OAQ
Kathmandu 2025 | Mwanajeshi wa Nepal aliyejeruhiwa kufuatia maandamano
Jeshi la Nepal (APF) wakimbeba mwenzao aliyejeruhiwa wakati wa maandamano ya kuipinga serikaliPicha: Prabin Ranabhat/AFP

Msemaji wa polisi nchini Nepal Binod Ghimire amesema kuwa idadi ya vifo kutokana na maandamano yaliyofanyika wiki hii nchini humo imefikia watu 51.

Watu hao wakiwemo waandamanaji 21, wafungwa tisa, maafisa watatu wa polisi na raia wengine 18 walifariki kutokana na maandamano ya wiki hii ya kupinga ufisadi.

Inaarifiwa pia kuwa karibu wafungwa 12,500 walitoroka gerezani hadi sasa bado wanasakwa. Hizo zilikuwa ghasia mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa huko Nepal tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na kukomeshwa kwa utawala wa kifalme mnamo mwaka 2008.

Rais wa Nepal Ramchandra Paudel na mkuu wa majeshi Jenerali Ashok Raj Sigdel watafanya mkutano muhimu leo Ijumaa ambao utawashirikisha wadau mbalimbali ili kumteua kiongozi wa mpito atakayekubaliwa na pande zote kwa ajili ya kuziba ombwe la utawala baada ya maandamano makubwa yaliyoiangusha serikali na kuliacha bunge likiwaka moto.

Watu 1,300 wajeruhiwa, wafungwa 12,500 watoroka 

Kulingana na taarifa iliyotolewa na mwandamanaji Kamal Giri, Jaji mkuu wa zamani ndiye anatarajiwa kutangazwa kuwa kiongozi wa mpito.

"Ili kutafuta suluhisho kutokana na hali ya sasa, mkuu wa majeshi na rais wameafiki kumteua jaji mkuu wa zamani Sushila Karki kuwa waziri mkuu wa serikali ya mpito, na hili ni jambo la kupongezwa sana."

Sushila Karki ambaye aliyekuwa mwanamke wa kwanza wa Nepal kuteuliwa katika nafasi hiyo mwaka 2016 ikiwa atateuliwa atasaidiwa na mwanaharakati mkuu wa kundi la vijana wanaofahamika zaidi kama "Gen Z" ambao ndio walikuwa mstari wa mbele kwenye maandamano hayo.

Kathmandu 2025 | Vurugu kufuatia maandamano ya vijana wa "Gen Z" huko Nepal
Gari lililoteketezwa moto kando mwa barabara mjini Kathmandu, NepalPicha: Skanda Gautam/ZUMA/IMAGO

Wakati baadhi ya vijana wakishinikiza pia kuvunjwa kwa Bunge, Rais Paudel ametoa taarifa kwa umma hapo jana jioni akisema kuwa "suluhisho la tatizo hilo linashughulikiwa haraka iwezekanavyo." Jeshi limeendelea kushika doria katika mitaa yenye utulivu ya mji mkuu Kathmandu kwa siku ya tatu mfululizo.

Taifa la Nepal lenye watu milioni 30 lilitumbukia katika machafuko makubwa wiki hii baada ya vikosi vya usalama kujaribu kusambaratisha mikusanyiko ya vijana waliokuwa wakiandamana kupinga ufisadi na kufungwa kwa mitandao ya kijamii.

Maandamano hayo yalipelekea Waziri Mkuu Khadga Prasad Oli kujiuzulu na kukimbia.

Maandamano hayo yalizidisha matatizo ya kiuchumi yanayolikumba taifa hilo masikini kwa muda mrefu ambapo kulingana na Bengi ya Dunia karibu theluthi moja ya vijana walio na umri kati ya miaka 15-24 hawana ajira.

Vyanzo:  AFP, Reuters