Perisic aiaga Dortmund, ajiunga na Wolfsburg | Michezo | DW | 07.01.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Perisic aiaga Dortmund, ajiunga na Wolfsburg

Wakati Ligi ya Ujerumani Bundesliga ikiwa katika mapumziko, shughuli za usajili wa wachezaji wapya zinaendelea, Kiungo Mcroatia Ivan Perisic amejiunga na klabu ya Wolfsburg kutoka Borussia Dortmund

Fußball Bundesliga Trainingslager VfL Wolfsburg: Vorbereitung Winterpause am 06.01.2013 im türkischen Kadriye (Belek). Wolfsburgs Neuverpflichtung Ivan Perisic spricht während einer Pressekonferenz. Foto: Soeren Stache/dpa pixel Schlagworte .Fußball , .Trainingslager , Training , sport , .Sport , Gestik , Winter , Ausland , Mannschaftssport , Belek , .Bundesliga , Vorbereitung , .lni , pk

Fußball Ivan Perisic VfL Wolfsburg Wechsel

Perisic, ambaye ameichezea timu yake ya taifa mechi 17 na hata kucheza mechi zote tatu za Dimba la Mataifa ya Ulaya UEFA euro 2012, alijiunga na Dortmund mnamo mwaka wa 2011 kutoka klabu ya Ubelgiji Bruges. Hata hivyo alijikuta nyuma ya wachezaji kama vile Marco Reus, Mario Götze na Kevin Grosskreutz katika nafasi ya kushiriki katika kikosi cha kwanza, na aliwahi kuanza mechi tatu pekee za ligi msimu huu. Kwingineko kiungo wa timu ya taifa ya Ujerumani Sven Bender na kiungo wa Serbia Neven Subotic wamekubali kuirefusha mikataba yao katika klabu ya Borussia Dortmund. Bender amekubali kuurfusha mkataba wake kwa mwaka mmoja hadi mwaka wa 2017, naye Subotic akiurefusha kwa miaka miwili hadi mwaka wa 2016. Bender mwenye umri wa miaka 23, na Subotic, miaka 24 wamejiunga na Mario Götze, Mats Hummels, Jakub Blaszczykowski, Mitch Langerak na Lukasz Piszczek katika kuirefusha mikataba yao na mabingwa hao watetezi wa Bundesliga.

Blatter amkosoa Boateng

Kevin-Prince Boateng alionyesha hasira kwa kuondoka uwanjani

Kevin-Prince Boateng alionyesha hasira kwa kuondoka uwanjani

Rais wa shirikisho la soka ulimwenguni FIFA Sepp Blatter anaamini kwamba mchambuliaji wa AC Milan Kevin-Prince Boateng alifanya vibaya kuondoka uwanjani wakati alipotolewa matamshi ya kibaguzi na mashabiki, ijapokuwa anasisitiza kuwa anaunga mkono vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Boateng alikabiliwa na matamshi ya kibaguzi kutoka kwa mashabiki wa klabu ya Pro Patria wakati wa mchuano wa kirafiriki siku ya Alhamisi iliyopita, nchini Italia, na mshambuliaji huyo Mghana ambaye mzaliwa wa Ujerumani akajibu kwa kuupiga mpira upande wa viti vya mashabiki na uondoka uwanjani akifuatwa na wachezaji wenzake wa Milan. Boateng mwenye umri wa miaka 25 amesisitiza kuwa ataondoka tena uwanjani kama atakabiliwa na tukio kama hilo bila kuzingatia umuhimu wa mchuano wa wakati huo. Lakini Blatter amesema huo ulikuwa uamuzi mbaya, akiongeza kuwa suluhisho la pekee ni kuweka adhabu kali, ikiwa ni kupunguza pointi, au kitu kingine sawa na hicho.

AFCON

Na sasa msikilizaji hebu tuangalie dimba la mataifa ya Afrika AFCON ambalo linaanza nchini Afrika Kusini tarehe 19 mwezi huu, na mengi yanaendelea katika kambi za mazoezi za timu zitakazoshiriki. Kocha wa Ghana Kwesi Appiah amemwacha nje ya kikosi chake kiungo Dede Andre Ayew. Mchezaji huyo wa Marseille Ufaransa, alipata jeraha la mguu wakati akifany amazoezi wiki iliyopita na akashindwa kujiunga na wachezaji wa Ghana katika kambi yao ya mazoezi mjini Abu Dhabi. Ghana wako katika kundi B dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mali na Niger.

The Super Eagles ni miongoni mwa timu zinazotarajiwa kufanya vizuri

The Super Eagles ni miongoni mwa timu zinazotarajiwa kufanya vizuri

Nigeria imemfungia mlango mshambulizi wa klabu ya Newcastle Shola Ameobi baada ya kukosa kuwasili mwishoni mwa wiki katika kambi ya maoezi nchini Ureno. Mkufunzi wa Newcastle Allan Pardew amesema Ameobi hatoshiriki dimba la AFCON. Naye kiungo wa CHELSEA John Obi Mikel amesema yuko katika hali nzuri tayari kushiriki katika kinyang'anyiro hicho. Mikel ambaye yuko na kikosi cha SuperEagles mjini Faro, Ureno, amekosa michuano ya karibuni ya Chelsea katika ligi na kombe la FA. Kikosi cha Nigeria kitakachoshiriki dimba la AFCON katika kundi C dhidi ya mabingwa watetezi Zambia, Burkina Fasi na Ethiopia, kitatajwa kesho, siku moja kabla ya Super Eagles kucheza mchuano wa kujipima nguvu dhidi ya Visiwa vya Cape Verde. Wakati huo huo, mabingwa watetezi Zambia wamekabiliwa na shinikizo kutoka kwa vyombo vya habari baada ya kushindwa mchuano wao wa kirafiki wa tatu mfululizo. Zambia walizabwa magoli mawili kwa sifuri dhidi ya Angola nchini Afrika Kusini. Uamuzi wa kocha Mfaransa Herve Renard wa kukibadilisha kikosi cha kwanza katika kipindi cha pili, haukuyafirahisha magazeti ya mjini Lusaka. Mwakilishi pekee wa Afrika mashariki, Ethiopia itachuana leo na Tunisia katika mchuano wa kuyanoa makali mjini Doha kabla ya kuelekea Afrika Kusini.

Tennis

Na katika mchezo wa tennis, wachezaji wanaoorodheshwa nambari moja ulimwenguni, Novak Djokovic na Victoria Azarenka leo wametajwa kuwa katika nafasi za kwanza, tayari kwa kinyang'anyiro cha wiki ijayo cha Australian Open mjini Melbourne. Djokovic, ambaye alimnyamazisha Rafael Nadal katika fainali ya mwaka jana iliyodumu seti tano, analenga kupata taji lake la tatu mfululizo la Australian Open. Roger Federer, ambaye ametwaa mataji makuu ya Grand Slam 17 katika fainali 24, amepangwa katika nafasi ya pili kabla ya bingwa wa kinyang'anyiro cha US Open, Andy Murray na Mhispania David Ferrer. Nadal atakosa kinyang'anyiro hicho kikuu cha kufungua mwaka kwa sababu ya kusumbuliwa na kirusi cha tumbo. Bingwa mtetezi katika upande wa wanawake Azarenka amepangwa mbele ya Mrusi Maria Sharapova aliyefika fainali mwaka jana, bingwa mara tano Serena Williams na Agnieszka Radwanska wa Poland ambaye alifika fainali ya Wimbledon.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters/DPA/AP

Mhariri: Yusuf Saumu