1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu zaidi ya 2000 wafukiwa na matope Papua New Guinea

27 Mei 2024

Serikali ya Papua New Guinea imesema zaidi ya watu 2000 wamefukiwa na maporomoko ya matope yalioharibu kijiji kizima, na kuomba msaada wa kimataifa katika juhudi zake za uokozi.

https://p.dw.com/p/4gKFI
Maporomoko makubwa Papua New Guinea
Mtu aliejeruhiwa akiwa amebebwa kwenye machela kutafuta matibabu baada ya kuokolewa kijiji cha Yambali, Papua New Guinea, Ijumaa, Mei 24, 2024.Picha: Benjamin Sipa/International Organization for Migration via AP/picture alliance

Sehemu kubwa ya kijiji cha Yambali kilichoko mkoa wa Enga ilifunikwa baada ya kuporomoka kwa mlima Mungalo majira ya asubuhi siku ya Ijumaa na kusomba majumba kadha na watu waliokuwa wamelala ndani yake.

Kituo cha kusimamia majanga cha Papua New Guinea kimesema katika barua yake kwa Umoja wa Mataifa kwamba maporomoko hayo ya matope yalifukia zaidi ya watu 2,000 wakiwa hai na kusababisha uharibifu mkubwa wa majengo, mashamba ya chakula na kuleta athari kubwa kwa uchumi wa taifa hilo.

Kituo hicho kimeiambia ofisi ya mratibu mkaazi wa Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Port Moresby kwamba hali inasalia kuwa tete huku matope yakiendelea kuhama taratibu, na kusababisha hatari inayoendelea kwa timu za uokozi pamoja na manusura.

Papua-New Guinea, Yambali | Maporomoko ya matope
Zoezi la ufukuaji kwa kutumia nyenzo duni.Picha: Mohamud Omer/International Organization for Migration/AP/picture alliance

"Nina wanafamilia 18 waliofukiwa chini ya vifusi na udongo ambao nimesimama juu yake, na wanafamilia wengi zaidi kijijini siwezi kuwahesabu," mkazi Evit Kambu aliiambia Reuters. "Lakini siwezi kufukua miili kwa hivyo nimesimama hapa bila msaada."

Zaidi ya saa 72 baada ya maporoko hayo, wakaazi bado wanatumia makoleo, vipande vvya mbao na mikono yao mitupu kujaribu kufukua vifusi ili kuwafikia manusura.

Soma pia: Maporomoko ya udongo yaua mamia ya watu Papua New Guinea

Vifaa vizito na misaada imechelewa kufika kutokana na umbali wa eneo la tukio huku vita vya kikabila vilivyo karibu vikiwalazimu wafanyakazi wa misaada kusafiri kwa misafara iliyosindikizwa na wanajeshi na kurejea katika mji mkuu wa mkoa, takriban kilomita 60 (maili 37) usiku.

Watu wasita kupokea vifaa vikubwa 

Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji nchini Papua New Guinea, Serhan Aktoprak, amesema baadhi ya wenyeji wamekuwa wakisita kupokea vifaa vikubwa vya kuondoa vifusi ili kutotatiza maombolezi ya wapendwa wao.

Shirika hilo limesema pia mazingira magumu ya eneo hilo na ugumu wa kufikisha misaada vinafifisha zaidi matumaini ya kupata manusura zaidi.

Ofisi ya Waziri Mkuu James Marape ilisema maafa hayo yanashughulikiwa na mamlaka ya dharura ya PNG na Marape alikuwa katika mji mkuu Port Moresby akijiandaa kurejea bungeni siku ya Jumanne, ambako anakabiliwa na hoja ya kutokuwa na imani naye.

Papua New-Guinea | Maporomoko ya matope Yambali.
Watu wakibeba mifuko kufuatia maporomoko ya matope katika kijiji cha Yambali, Mkoa wa Enga, nchini Papua New Guienea, Mei 24, 2024.Picha: Andrew Ruing/REUTERS

Msaada wa kimataifa

Rais wa China Xi Jinping amesema leo kuwa amehuzunishwa na taarifa za janga hilo la maporomoko nchini Papua New Guinea, na kuahidi kutoa msaada kwa taifa hilo la kanda ya Pasifiki.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje ya China Mao Ning, amesema mjini Beijing kwamba China itatoa msaada ulio ndani ya uwezo wake kwa ajili ya shughuli za uokozi wa ujenzi mpya kulingana na mahitaji ya Papua New Guinea.

Mkuu wa shirika la afya duniani, WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, pia ameelezea kuhuzunishwa na janga hilo na kuahidi kupitia mtandao wa kijamii wa X kwamba shirika hilo liko tayari kusaidia, huku Australia ikitangaza kuwa tayari kupeleka vifaa vizito kwa ajili ya ufukuaji.

Chanzo: Mashirika