1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiPapua New Guinea

Waokoaji wapambana kuwatafuta manusura Papua New Guinea

27 Mei 2024

Waokoaji wanaendelea kupambana kuwatafuta manusura baada ya maporomoko ya udongo kukiangamiza kijiji kimoja nchini Papua New Guinea na kuwauwa karibu watu 670.

https://p.dw.com/p/4gJF7
Maporomoko ya udongo Papua New Guinea
Shughuli za uokozi zianaendelea katika eneo la Yambali, Papua New Guinea kufuatia maporomoko ya udongoPicha: Mohamud Omer/International Organization for Migration/AP/picture alliance

Kijiji hicho kilichoko kando ya mlima katika mkoa wa Enga kiliangamizwa karibu chote wakati kipande kikubwa cha Mlima Mungalo kiliporomoka Ijumaa alfajiri, na kuzifukia nyumba na watu waliokuwa wamelala.

Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa amesema tayari siku tatu zimeisha tangu mkasa huo kutokea kwa hiyo wanakimbizana na muda kuona kama wanaweza kuwaokoa manusura wowote. Amesema waokoaji wanakabiliwa na mazingira magumu na hatari kwa sababu miamba inaendelea kuanguka na kutatiza shughuli zao. Ameongeza kuwa kuna maji yanayotiririka chini ya vifusi hali ambayo inafanya ardhi kuwa telezi. Watu kutoka karibu nyumba 250 zilizoko karibu wamehamishwa kama hatua ya tahadhari.

Mashirika ya misaada na viongozi wa eneo hilo awali walihofia kati ya watu 100 na 300 waliangamiachini ya tope na vifusi kwenye eneo la ukubwa wa karibu viwanja vinne vya kandanda. Lakini idadi hiyo iliongezeka hadi 670 baada ya viongozi wa eneo hilo na wafanyakazi wa masuala ya dharura kugundua kuwa takwimu rasmi zilikuwa zimeipunguza idadi ya wakaazi.