Papa Francis awasili Ufilipino | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.01.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Papa Francis awasili Ufilipino

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis, amewasili nchini Ufilipino, nchi yenye Wakatoliki wengi zaidi barani Asia, huku ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa.

Papa Francis

Papa Francis

Maelfu ya Wafilipino wamejipanga katika misururu mirefu kwenye barabara za mji mkuu wa Ufilipino, Manila, wakimkaribisha kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani anayezuru nchini humo kwa siku tano, akitokea nchini Sri Lanka. Serikali ya Ufilipino imetangaza kwamba wakati wote wa ziara ya Papa Francis, nchi hiyo itakuwa katika mapumziko ya kitaifa na pia imepiga marufuku ya pombe.

Papa atakuwa katika mji mkuu, Manila na mwishoni mwa juma atakwenda kwenye jimbo la mashariki la Leyte, ambapo anatarajiwa kukutana na wahanga wa kimbunga Haiyan, kilichoikumba nchi hiyo mwaka 2013.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Manila, Mwadhama Luis Kardinali Antonio Tagle amesema ziara ya Papa inafanyika wakati ambapo watu watapata msaada wa kiroho na kimaadili. Kardinali Tagle, amesema makanisa kuzunguka nchi nzima yatapiga kengele kwa wakati mmoja katika hatua ya kumkaribisha kiongozi huyo.

Papa Francis akiongoza Misa Colombo 14.01.2015

Papa Francis akiongoza Misa Colombo 14.01.2015

Amesema wameridhishwa na kufurahishwa na ulinzi uliopo, lakini amewasihi watu wa usalama kutomtenganisha Papa na watu wake. Amesema Papa Francis ni mchungaji, hivyo anahitaji kuwa pamoja na kundi la watu wake.

Papa kukutana na Rais Aquino

Papa Francis atakutana pia na Rais Benigno Aquino, ambaye aliwahi kuwa katika mvutano mkali na viongozi wa Kanisa Katoliki kutokana na muswada wa afya ya uzazi uliokuwa unahamasisha matumizi mbalimbali ya kinga ya uzazi wa mpango. Hata hivyo, Bunge la Ufilipino lenye washirika wengi wa Rais Aquino, waliupitisha muswada huo mwaka 2012, ambao ni kiunyume na Kanisa Katoliki.

Mkuu wa Majeshi wa Ufilipino, Jenerali Gregorio Catapang, amesema kwa mwaka huu kutakuwa na ulinzi mkali kuliko ilivyo kawaida na kwamba kiasi watu milioni sita wanatarajiwa kuhudhuria Ibada ya Misa itakayofanyika siku ya Jumapili mjini Manila.

Rais Benigno Aquino wa Ufilipino

Rais Benigno Aquino wa Ufilipino

Jenerali Catapang amesema karibu wanajeshi na askari polisi 40,000 wametawanywa kwa ajili ya kumlinda Papa Francis wakati wa ziara yake. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufilipino, Mar Roxas amesema wanatarajia kuwa msafara wa Papa utazunguza kwa muda wa saa tatu, ili kuweza kushuhudiwa na karibu watu nusu milioni.

Akiwa nchini Sri Lanka, Papa Francis alisema dini kamwe haiwezi kuwa kisingizio cha kufanya vurugu na kwamba maridhiano hayawezekani bila ukweli kubainishwa. Papa aliutembelea msitu mnene kaskazini mwa nchi hiyo katika kuonyesha mshikamano na wahanga wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 25.

Papa Francis ni Papa wa tatu kuzuru Ufilipino. Mwaka 1995 kiasi Wakatoliki milioni nne walihudhuria Ibada ya Misa iliyoadhimishwa na Papa Yohane Paulo wa Pili katika uwanja wa Rizal, na hivyo kuwa umati mkubwa kabisa kuwahi kushuhidiwa katika matukio yote ya Papa. Aidha, mnamo mwaka 1970, Papa Paulo wa Sita, alizuru Ufilipino.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com