Papa Francis awaita wakimbizi kwa jina lao ″warohingya″ baada ya mkutano Bangladesh | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.12.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Papa Francis awaita wakimbizi kwa jina lao "warohingya" baada ya mkutano Bangladesh

Papa Francis ameomba msamaha kutoka kwa wakimbizi nchini Bangladesh kwa madhila waliyoyahimili, akidai haki zao zitambuliwe na akatamka neno ambalo amekuwa akiliepuka siku chache tu huko nchini Myanmar la "rohingya."

Akikutana na kikundi cha warohingya ijumaa hii, papa Francis aliwasalimu na kuwabariki wakimbizi hao, akiwafariji kwa kuwashika mikono na kusikiliza hadithi zao katika hatua ya kuonyesha mshikamano pamoja nao dhidi ya kitendo kibaya zaidi cha wakimbizi kuwahi kuonekana barani Asia.

Papa aliomba radhi kutokana na kugawanyika kwa walimwengu kuhusiana na kadhia iliyowafika warohingya na kisha akatamka jina la kabila lao mbele ya viongozi wa kidini waliokusanyika wa kiislamu, wabudha, wahindu na wakristo.

Warohingya 16 – wanaume 12, wanawake wawili wasichana wawili walisafiri jijini Dhaka, mji mkuu wa Bangladesh kutoka Cox's bazar, wilaya inayopakana na Myanmar ambako kambi ya wakimbizi zimefurika kupita kiasi kukiwa na zaidi ya warohingya 620,000 waliokimbia kile umoja wa mataifa inachosema ni kampeni ya safisha safisha ya kikabila inayofanywa na jeshi la Myanmar.

Kampeni hiyo ambayo ni pamoja na kuvichoma moto vijiji vya warohingya inahusu pia kuteswa; kubakwa na kupigwa risasi na wanajeshi wa Myanmar na makundi ya waumini wa budha. Kutokana na yote haya hawakuwa na chaguo lengine isipokuwa kufanya safari za hatari na wengine hata kufariki njiani wakipita kwenye misitu na kwa njia ya bahari hadi Bangladesh.

Serikali ya Myanmar imekanusha kuna kampeni ya aina hii. Nchi hiyo ambayo wakazi wake wengi ni wafuasi wa dini ya budha inadai kwamba warohingya waislamu walio wachache ni Wabengali waliohamia Myanmar kinyume cha sheria kutoka Bangladesh.

Myanmar haiwatambui kuwa ni kabila dogo la wachache na inawanyima hata uraia ingawa wameishi nchini humo tangu vizazi na vizazi.

Bangladesch Dhaka - Papst Franziskus besucht Rohingya Flüchtlinge (Reuters/M. Rossi)

Papa Francis akikutana na wakimbizi warohingya huko nchini Bangladesh

Wakimbizi hao walimsongelea papa Francis mmoja baada ya mwengine baada ya hafla ya ijumaa ya leo, naye akambariki msichana mmoja mdogo akimwekea mkono kichwani na kumshika begani mvulana mmoja.

Papa Francis aliwaambia wakimbizi hao na hapa ninanukuu; "huenda hatuna kubwa la kuwafanyia lakini janga lenu linatugusa moyoni: kwa wale waliowaumiza na zaidi ya yote tofauti zilizopo duniani nawaomba msamaha.”

Kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani akatoa wito wa kuendelea kuwatetea warohingya ili haki zao ziweze kutambuliwa.

Kwa sababu ya kidiplomasia wakati alipokuwa Myanmar papa Francis alijizuia kutamka neno "Rohingya" kuepusha mzozo wa kidiplomasia na wenyeji wake.

Kukutana kwake na wakimbizi nchini Bangladesh kumekamilisha shughuli zake za leo zilizoanza na misa ya kuwatawaza mapadri wapya 16.

Jamii ndogo ya wakatoliki nchini Bangladesh ni asilimia moja tu ya wakazi mia moja sitini milioni ya nchi hiyo ambao wengi ni waislamu.

Licha ya idadi ndogo ya wakristo; kanisa katoliki lina mlolongo wa shule, nyumba za yatima na zahanati na limeendesha shughuli zake kwa uhuru.

Mwandishi: Fathiya Omar/ape

Mhariri:Josephat Charo

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com