1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis aongoza Misa ya Jumapili ya Matawi

2 Aprili 2023

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis ameongoza misa iliyohudhuriwa na umati wa waumini wa Kanisa Katoliki kwenye uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Petro kuadhimisha Jumapili ya matawi

https://p.dw.com/p/4PbYX
Vatikan | Palmsonntagsmesse
Picha: Andrew Medichini/AP Photo/picture alliance

Papa Francis ameongoza misa hiyo muda mfupi baada ya kutoka hospitali ambako alilazwa. Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki aliwapungia waumini wapatao 30,000 kutokea kwenye gari lake.

Jumapili ya matawi ni siku ya kukumbuka kuwasili kwa Yesu mjini Jerusalem kabla ya kusulubiwa. Pasaka itakuwa tarehe 9 Aprili ambayo ni siku ya kuadhimisha kufufuka kwa bwana Yesu.

Baba mtakatifu amewataka waumini kutowapuuza wale wanaokabiliwa na dhiki kubwa na upweke. Amesema idadi ya watu hao ni kubwa. Amesikitika kwamba watu wanadhulumiwa na kutelekezwa.

Papa Francis amesema wahamiaji sasa siyo binadamu bali wamekuwa takwimu. Ameeleza kuwa watu wanatupiliwa mbali na matatizo yao.

Vatikan | Palmsonntagsmesse
Maelfu ya waumini walifika katika uwanja wa Mtakatifu Petro kwa Misa ya Jumapili ya MatawiPicha: Gregorio Borgia/AP Photo/picture alliance

Papa Francis ambaye ni mtu mzima alikaa chini wakati wote wa misa na kumwachia kadinali aongoze shughuli zote kutokea kwenye madhabahu.

Kiongozi wa Kanisa katoliki amewashukuru wote waliomwombea wakati alipokuwa anaugua. Papa Francis mwenye umri wa miaka 86 alilazwa hospitalini mnamo siku ya Jumatano akiwa na matatizo ya kupumua hali iliyozua wasiwasi kwamba huenda angeshindwa kuhudhuria mfululizo wa ibada katika wiki muhimu zaidi katika kalenda ya Kikristo.

Baba mtakatifu alifanya utani kwa kusema "bado ni hai” baada ya kutoka hospitali anakabiliwa na matatizo ya kiafya, ikiwa pamoja na maumuvi ya kwenye goti yaliyosababisha atumie kiti cha magurudumu na mkongojo.

Makao makuu ya Vatican yamesema sasa baba mtakatifu hawezi kusimama kwa muda mrefu.

Madhila yake ya kiafya yamesababisha wasi wasi na uvumi kwamba huenda akaamua kustaafu. Hata hivyo kwa sasa hana mpango wa kungàtuka.

Mapema mwezi huu Papa Francis aliadhimisha mwaka wa 10 tangu awe mkuu wa Kanisa Katoliki. Katika kipindi hicho  amepitisha mageuzi makubwa kwa lengo la kuleta uwazi na upendo zaidi kwenye Kanisa Katoliki licha ya kukabiliwa na upinzani wa wahafidhina.  

afp, dpa, reuters,ap