1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis akiri kufanya makosa kashfa ya udhalilishaji

Sylvia Mwehozi
12 Aprili 2018

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amekiri kuwa alifanya makosa makubwa namna alivyoshughulikia kashfa ya udhalilishaji wa kingono nchini Chile. 

https://p.dw.com/p/2vwdr
Vatikan Papst Franziskus
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Medichini

Katika barua yake kwa maaskofu 32 wa Chile iliyotolewa na Vatican, Papa Francis amesema anadhamiria kuwaita maaskofu hao mjini Roma ili kujadiliana juu ya uchunguzi  wa madai ya kumlinda askofu Juan Barros dhidi ya udhalilishaji uliofanywa na padri Fernando Karadima katika miaka ya 1980 na 90.

Papa Francis ameelezea "aibu" yake na "maumivu" ya mateso waliyopitia waathirika na kuahidi kukutana nao. Msemaji wa Vatican Greg Burke amewaambia waandishi wa habari kuwa "Papa katika barua yake kimsingi anafanya tendo kubwa la unyenyekevu. Anasema, "nimefanya kosa, anasema binafsi nataka kuomba msamaha kwa wote niliowakosea na nitawaita maaskofu wote wa Chile waje hapa tujadili kipi cha kufanyia mabadiliko. Anazungumizia hatua za muda mfupi, kati na muda mrefu. kwahiyo kutakuwa na mabadiliko katika kanisa huko Chile."

Chile Bischof Juan Barros währen der Papstmesse in Iquique
Askofu Juan Barros anayedaiwa kushuhudia udhalilishaji wa kingonoPicha: Reuters/A. Bianchi

Hakumtaja Barros, ambaye alichaguliwa kama askofu wa Osorno nchini Chile licha ya kutuhumiwa kwamba alificha na hata kushuhudia udhalilishaji uliofanywa na Karadima. Ripoti ya kurasa 2,300 iliyotumwa kwa Papa inajumuisha ushahidi uliokusanywa kutoka kwa watu 64 jijini New York na Santiago. 

Papa amewaita maaskofu mjini Roma ili kujadili juu ya matokeo ya uchunguzi uliofanywa na askofu Charles Scicluna na kutaka "ushirikiano na usaidizi" katika hatua zinazoweza " kusafisha kashfa hiyo kwa haraka na kuleta haki.

Wakati wa ziara yake nchini Chile mwezi Januari, kiongozi huyo alimtetea vikali Barros, aliyeonekana katika ibada za umma zilizoendeshwa na Papa katika miji mitatu ya Chile, na kuchochea hasira ya umma. Francis anasema kwamba aliamini Barros hakuwa na hatia na kutaka "ushahidi" wa udhalilishaji kabla ya kuzungumza dhidi yake.

Vatikan maltesischer Erzbischof Charles Scicluna
Charles Scicluna aliyekusanya ushahidi nchini Chile juu ya udhalilishaji wa kingonoPicha: picture-alliance/AP Photo/G. Borgia

Hata hivyo, baadae aliomba msamaha kwa waathirika na kumtuma Scicluna, mchunguzi mpya wa Vatican kwenda Chile kukusanya ushahidi. Scicluna alirejea mwezi Februari. Karadima, padri mwenye ushawishi nchini Chile, alihukumiwa na Vatican mwaka 2011 kwa kuwadhalilisha vijana wa kiume na kufungwa kifungo cha maisha. Mashitaka dhidi yake katika mahakama za Chile yalitupiliwa mbali kwasababu ya kukosekana ushahidi.

Rais wa mkutano wa maaskofu wa Chile, askofu Santiago Silva amesema kanisa halijafanya vya kutosha, akiongeza kwamba lengo lao ni kwamba hilo halitojitokeza tena. Silva amesema mkutano wa maaskofu wa Chile na Papa mjini Roma utafanyika wiki ya tatu ya mwezi Mei.

Tangu achukue uongozi wa kanisa hilo machi 2013, Papa Francis amekuwa mtetezi wa tabaka la watu wanaotwezwa na kuanzisha ajenda ya mageuzi. Hata hivyo kashfa za udhalilishaji wa ngono umegubika uongozi wake na Vatican ilitangaza kufufua jopo lake dhidi ya watu wanaovutiwa na watoto kingoni mwezi februari.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/afp

Mhariri: Iddi Ssessanga