Papa Francis aitaka Ufilipino kupambana na rushwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.01.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Papa Francis aitaka Ufilipino kupambana na rushwa

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis, ameitaka serikali ya Ufilipino kupambana na tatizo kubwa la rushwa iliyokithiri nchini humo, na amewataka viongozi kumaliza kabisa umaskini.

Rais Benigno Aquino, akisalimiana na Papa Francis

Rais Benigno Aquino, akisalimiana na Papa Francis

Papa Francis ameitoa kauli hiyo leo, katika hotuba yake ya kwanza wakati wa ziara yake ya siku tano nchini Ufilipino, ambayo asilimia 88 ya wananchi wake ni Wakatoliki, mara baada ya kuwasili hapo jana na kupokelewa na Rais Benigno Aquino. Akizungumza katika Ikulu ya rais wa Ufilipino huko Malacanang, Papa amesema umefika wakati kwa viongozi wa kisiasa kuzingatia uadilifu, uaminifu na kujitolea kwa maslahi ya watu wote, na kusikia kilio cha mamilioni ya wananchi wake walio maskini na hivyo kuleta haki sawa za kijamii.

''Wasaidieni wale wanaoishi katika jamii iliyoathirika kwa umaskini na rushwa, waliokata tamaa ya kiroho, wanaokuwa kwenye majaribu ya kutaka kuacha shule na kuishi mitaani. Wafilipino wanajulikana kila mahali kwa upendo wao kwa Mungu, na kujitoa kwao kwa Mama Maria pamoja na Rozari yake, alisema Papa Francis.''

Watu wakipunga mkono kumsalimu Papa, Manila

Watu wakipunga mikono kumsalimu Papa, Manila

Amewasihi wananchi wote wa Ufilipino na katika ngazi zote kukataa aina yoyote ya rushwa, ambayo inachangia kuchukua rasilimali kutoka kwa watu maskini. Papa amesema inawapasa watu kuondokana na ukandamizaji na dhuluma, ambavyo kwa pamoja husababisha kutokuwepo kwa haki sawa miongoni mwa jamii.

Tatizo la rushwa limeikumba Ufilipino tangu enzi za utawala wa miaka 20 wa aliyekuwa dikteta wa nchi hiyo, Hayati Ferdinand Marcos, ambaye pamoja na mkewe, aliyekuwa akipenda maisha ya kifahari, walituhumiwa kuiba kati ya Dola bilioni tano na Dola bilioni kumi, kabla hajaondolewa madarakani mwaka 1986.

Rais Aquino aliahidi kupambana na rushwa

Rais Aquino mtetezi wa demokrasia na mtoto wa rais wa zamani wa Ufilipino, Corazon Aquino, aliingia madarakani mwaka 2010, huku akiahidi kuwa na serikali yenye uwazi, utawala bora pamoja na kupambana na tatizo la rushwa kwa lengo la kuwatoa Wafilipino katika dimbwi la umaskini.

Baada ya kukutana na Rais Aquino, Baba Mtakatifu aliongoza Ibada ya Misa katika Kanisa Kuu la Manila. Baada ya Ibada hiyo, Papa Francis alikutana na watoto wa mitaani, ambapo alitumia muda wa dakika 20 kuwasikiliza, kuimba pamoja nao na kubadilishana zawadi.

Papa Francis akiwapungia mkono watu waliofurika kumlaki, Manila

Papa Francis akiwapungia mkono watu waliofurika kumlaki, Manila

Baadaye leo, Papa Francis atakutana na familia za Wafilipino. Aidha, kesho atakwenda kwenye jimbo la mashariki la Leyte, ambapo anatarajiwa kukutana na kuwafariji wahanga wa kimbunga Haiyan, kilichoikumba nchi hiyo mwaka 2013. Kimbunga hicho kilisababisha vifo vya zaidi ya watu 7,300 na kuviangamiza kabisa vijiji kadhaa.

Ulinzi mkali umeimarishwa wakati wa ziara ya Papa Francis, katika historia ya Ufilipino, ambapo kiasi wanajeshi na askari polisi 50,000 wametawanywa. Rais Aquino amemueleza Papa kuwa ulinzi kama huo haujawahi kutokea nchini humo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE,APE
Mhariri: Yusuf Saumu

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com