Palipo na utawala wa Mwanamke
Kuna mataifa huru 195 duniani, na mengi yanatawaliwa na wanaume. Wanawake watawala ni wachache, lakini wale walioko mamlakani ni majasiri. DW inawaangazia baadhi ya wanasiasa wanawake wenye ushawishi mkubwa.
Angela Merkel
Ana miaka 62, alichaguliwa kuwa Kansela mwaka 2005 na kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza serikali. Hivi sasa anapigania kuongoza awamu ya nne. Binti huyo wa mchungaji kutoka Mashariki ya Ujerumani na anayehodhi shahada ya udaktari wa Kemia, alitajwa kuwa "Mtu mashuhuri wa mwaka 2015" na gazeti la Time. Wakati kukiongezeka kwa siasa za kizalendo, vyombo vya habari vimemuita kiongozi wa dunia huru.
Theresa May
Theresa May ni Waziri Mkuu wa pili mwanamke wa Uingereza baada ya Margaret Thatcher wa miaka ya 1980. Ana miaka 60 na waziri wa zamani wa mambo ya ndani alichukua madaraka Julai 2016, wiki chache kabla ya kura ya BREXIT, na kuongoza mazungumzo ya kutoka EU. Kwa muda gani atasalia madarakani, bado ni swali, ingawa uchaguzi wa mapema wa Juni 2017 unaweza kuwa mwanzo wa kutoka madarakani.
Tsai Ing-wen
Tsai Ing-Wen ni mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Jamhuri ya China, inayojulikana zaidi Taiwan. Kuapishwa kwake mwezi Mei 2016 kuliifanya Beijing kusitisha mahusiano na kisiwa hicho kidogo, ambacho eneo la Bara linadai hakitawahi kuwa huru. Tsai tayari ameweka wazi kwamba "hatababaishwa na shinikizo hilo", linalohusiana na uhuru. Tsai pia ni Mwenyekiti wa chama cha Democratic Progressive Party.
Ellen Johnson Sirleaf
Mama huyu wa miaka 78 alichukua madaraka kama Rais wa Liberia tangu mwaka 2006. Ni mwanamke wa kwanza Barani Afrika kuwa kiogozi wa nchi. Mwaka 2011, Sirleaf na wanawake wengine wawili wanaharakati kutoka Liberia na Yemen walitunukiwa tuzo ya Nobel kwa harakati zao za kuhakikisha usalama kwa wanawake na haki za wanawake kushiriki kikamilifu katika michakato ya kuleta amani.
Dalia Grybauskaite
Dalia Grybauskaite ni mwanamke wa kwanza kuongoza taifa dogo la Baltika la Lithuania. Mara nyingi amekuwa akichukuliwa kama "Mwanamke wa chuma" kwa sababu ana mkanda mweusi wa mchezo wa Karate na si mtu wa kuzungumza upuuzi. Mwanamama huyu wa miaka 61 ameshika vyeo mbalimbali serikalini kabla ya kuchaguliwa kuwa rais mwaka 2009 na kuchaguliwa tena mwaka 2014.
Erna Solberg
Norway, pia inaongozwa na mwanamke. Erna Solberg aliingia madarakani mwaka 2013. Solberg mwenye miaka 56 ni mwanamke tajiri, anayetokea Kaskazini mwa nchi hiyo na waziri mkuu wa pili baada ya Gro Harlem Brundtland. Sera zake kali kuhusu hifadhi zimempatia jina la utani "Erna wa Chuma". Erna pia anaongoza chama cha Conservative cha Norway.
Beata Szydlo
Waziri mkuu wa tatu mwanamke wa Poland. Amekuwa madarakani tangu Novemba 2015. Alilieleza bunge kwamba vipaumbele vya serikali yake ni usalama wa raia wa poland na mchango wa taifa hilo kwa masuala ya usalama wa EU. Mwanamke huyo ana umri wa miaka 54, kabla ya kuwa waziri mkuu, alitumika kama meya na mwakilishi wa bunge.
Saara Kuugongelwa-Amadhila
Ana miaka 49 na waziri mkuu wa nne wa Namibia. Alichukua madaraka tangu 2015. Kuugongelwa-Amadhila aliishi uhamishoni nchini Sierra Leone tangu akiwa mdogo. Alisoma masomo yake ya juu nchini Marekani, na kupata shahada ya uchumi kabla ya kurejea nyumbani mwaka 1994, ambako alianza kujihusisha na siasa. Ni mwanamke wa kwanza kuongoza serikali ya Namibia na mpiganiaji mkubwa wa haki za wanawake.
Michelle Bachelet
Michelle Bachelet amekuwa rais wa Chile tangu 2014. Ni awamu yake ya pili: Tayari alikuwa Rais wa Chile wa kwanza mwanamke kutoka mwaka 2016-2010. Baada ya kuteseka kwa kifungo na mateso wakati akiwa mwanamke mdogo nchini Chile, aliishi miaka mingi uhamishoni Australia na Ujerumani Mashariki, ambako alisomea madawa. Baada ya kurejea Chile mwaka 1979, alianzisha vuguvugu la mpito wa demokrasia.
Sheikh Hasina Wajed
Gazeti la biashara la Forbes pia lilimtaja Waziri mkuu huyu wa Bangladesh katika orodha ya wanawake 100 wenye ushawishi kwa mwaka 2016. "Sheikh Hasina Wajed ana mamlaka kwenye nchi yenye idadi kubwa ya watu, ikiwa ni ya nane duniani, ina watu Milioni 162, na alichukua mamlaka haya tangu 2009, "Forbes liliandika kuhusu mama huyu mwenye miaka 69, ambaye amekuwa katika siasa kwa miongo kadhaa.
Kolinda Grabar-Kitarovic
Akiwa na miaka 49, tayari ameshika madaraka tofauti serikalini na kuwa balozi wa Croatia nchini Marekani kabla hajachaguliwa mwaka 2015 kuwa rais wa kwanza mwanamke, na umri wake mdogo. Nafasi ya Grabar-Kitarovic kuanzia 2011 hadi 2014 kama katibu mkuu msaidizi wa masuala ya diplomasi ya umma katika NATO kunamfanya kuwa mwanamke aliyeshika wadhifa wa juu zaidi katika timu ya uongozi ya NATO.