1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

kuuawa Osama Bin Laden ndiyo suluhisho.

Abdu Said Mtullya9 Desemba 2009

Jenerali wa Marekani asema lazima Osama bin Laden auawe ili kuweza kuwashinda Al-Qaeda.

https://p.dw.com/p/KyM7
Kamanda mkuu wa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan Jenerali McChrystal.Picha: AP

Kamanda mkuu wa majeshi ya NATO nchini   Afghanistan jenerali  Stanley McChrystal  amesema njia pekee ya kuwashinda magaidi  wa Al-Qaeda ni kuuliwa  au kukamatwa kwa Osama bin Laden.

Jenerali McChrystal amesema hayo leo mbele ya wabunge wa Marekani wakati akifafanua shabaha za uamuzi wa rais Obama   wa kupeleka askari  30,000 zaidi nchini  Afghanistan.

Jenerali McChrystal  amesema ongezeko la askari litachangia katika kurudisha nyuma vuguvugu la Al-Qaeda  hadi itakapofika  wakati kama huu hapo mwakani na kuwatenga kabisa na wananchi wa  Afghanistan.

Akifafanua mkakati mpya  wa Marekani wa  kuongeza majeshi nchini  Afghanistan jenerali McChrystal alisema kwamba Osama bin Laden ndiyo mvuto wa Al-Qaeda kwa sasa,na kuendelea kwake kuishi kunawaimarisha  Al-Qaeda hao  na kuwawezesha kuwa na nguvu  duniani.

Jenerali huyo amesema kuuawa au kukamatwa kwa Osama bin Laden hakutakuwa mwisho wa Al-Qaeda lakini ameeleza kwamba hafikiri iwapo itawezekana  kuwashinda  Al-Qaeda bila ya kuuawa au  kukamatwa kwa Osama bin Laden.

Maafisa wa Marekani  wanaamini kwamba Osama bin Laden anaesadikiwa kuwa alipanga mashambulio ya kigaidi ya terehe 11  mwezi septemba mwaka 2001nchini Marekani   amejificha katika sehemu za milimani , kwenye mpaka baina ya Pakistan na  Afghanistan.

Mshauri wa usalama  wa taifa nchini Marekani   James Jones alisema mwishoni  mwa wiki iliyopita kwamba taarifa za upelelezi  za hivi karibuni zinadokeza  kuwa Osama bin  Laden anaweza kuwa katika jimbo la Waziristan ya kaskazini- wakati mwingine katika upande  wa Pakistan na wakati mwingine katika upande wa  Afghanistan.

Hatahivyo  waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates alisema katika mahojiano hivi karibuni kwamba Marekani haijui wapi Osama bin Laden anaweza kuwapo.

Jenerali Mchrystal amesema  ana matumaini  juu ya  kuwashinda  taliban nchini  Afghanistan.  Amesema hadi mwaka  2011  itakuwa wazi kwa watu wa Afghanistan  kwamba  taliban hawatashinda.

Mwandishi Mtullya Abdu/ AFPE

Mhariri/Abdul-Rahman