Odinga adai mitambo ya IEBC ilidukuliwa | Uchaguzi Mkuu wa Kenya 2017 | DW | 09.08.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Kenya Yaamua

Odinga adai mitambo ya IEBC ilidukuliwa

Mgombe urais wa upinzani Kenya, Raila Odinga, adai mtambo wa kielectroniki ya tume ya uchaguzi (IEBC) ulidukuliwa na kura kuchakachuliwa akikitupia lawama chama tawala cha Jubilee.

Odinga amesema Jumatano kwamba kompyuta za tume ya uchaguzi ya Kenya zilifanyiwa udukuzi na matokeo ya uchaguzi yanayoendelea kutangazwa mtandaoni ni ya uongo, yanayomuonesha Rais Uhuru Kenyatta akiongoza katika kile alichokitaja kuwa ni 'udanganyifu mkubwa sana.'

"Udaganyifu uliofanywa na chama cha Jubilee dhidi ya raia wa Kenya umepindukia wizi wa kura wa wakati wowote katika histori ya nchi yetu. Lakini mara hii tumewakamata," ameandika Odinga katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Odinga, hata hivyo amesema wadukuzi walitumia taarifa za aliyekuwa meneja wa teknolojia wa IEBC Christopher Msando aliyeuawa wiki moja iliyopita ili kuingia katika mitambo ya IEBC.

Mnamo tarehe 31 Julai maafisa wa Kenya walitangaza kwamba Msando alikamatwa na kuteswa hadi kifo, na kuzua taharuki miongoni mwa wananchi wa Kenya waliokuwa na hofu ya kutokea tena machafuko ya kisiasa yaliyochochewa na mgawanyiko wa kikabila baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Kabla ya kifo chake,Msando, aliwahakikishia wapiga kura kwamba matokeo ya uchaguzi wa mara hii hayatachezewa.

Kenia Nairobi Wahlen Stimmenauszählung (Reuters/T. Mukoya)

Afisa wa usalama na afisa wa IEBC wakifanya kazi pamoja katika kituo cha kupigia kura cha Jamuhuri High School

Kwa upande wa IEBC, mwenyekiti wake Wafula Chebukati amesema anauamini mfumo wa mawasiliano ya kiteknolojia wa IEBC huo lakini madai yatashughulikiwa. Rafael Tuju ambaye ni afisa wa ngazi ya juu katika chama cha Kenyatta, amesema madai ya upinzani hayana msingi.

Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, amesema tume itayafanyia uchunguzi madai hayo ya Odinga, lakini kwa sasa haiwezi kutoa tamko lolote iwapo mtambo wa IEBC ulifanyiwa udukuzi au la.

Odinga pia ameyakataa matokeo ya awali yaliyotolewa kupitia katika mtambo huo yanayomuonyesha mpinzani wake Uhuru Kenyatta akiongoza kwa kura nyingi zaidi.

Taarifa za hivi karibuni za tume ya uchaguzi, Kenyatta anaongoza kwa asilimi 54.4 na Odinga anayo asilimi 44.77 baada ya kura kuhesabiwa katika zaidi ya vituo 39,320 kati ya vituo vyote 40,883.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ap/rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com