1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama azungumzia mkakati mpya nchini Afghanistan

23 Machi 2009

Asisitiza juu ya haja ya kuwa pia na mpango wa kuondoa.

https://p.dw.com/p/HHew
Rais Barack ObamaPicha: AP

Rais Barack Obama wa Marekani amesema nchi yake lazima iwe na "mkakati wa kuondoka Afghanistan", hata ikiwa inaongeza idadi ya wanajeshi wake nchini humo, kuimarisha harakati za kupambana na waasi wa Taliban.

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha televisheni cha CBS jana yaliodumu muda wa saa moja Rais Obama alisema " Hapana budi paweko na mpango wa kuondoka, lakini ieleweke kwamba haina maana kwamba kuna mvutano."

Matamshi hayo ya rais wa Marekani yamekuja katika wakati ambao anajiandaa kutangaza mkakati mpaya kuhusu Afghanistan dhidi ya ongwezeko la hujuma kutoaka kwa wapiganaji wa Taliban, jambo ambalo limezusha masuali juu ya juhudi za miaka saba sasa zinazoongozwa na Marekani kuunda taasisi za kidemokrasi nchini Afghanistan.

Obama alisema uamuzi wa mwezi uliopita kutuma wanajeshi wa ziada 17,000 wa Marekani nchini Afghanistan, kwa sehemu kubwa ikiwa ni kupambana na machafuko wakati wa uchaguzi ujao mwezi Agosti, ni uamuzi mgumu kabisa ambao amepaswa kuchukua tangu ashike rasmi madaraka ya kuliongoza taifa hilo kubwa.

Alisema ni jambo muwafaka , lakini lazima uamuzi huo ulinganishwe na hali halisi nkwa kutathimini mkakati unaochukuliwa wakati huu. Akaongeza kwamba ingawa makamanda wa kijeshi wa Marekani wamesema kutahitajika akaribu wanajeshi 30,000 wa ziada kukabiliana na hali mbaya katika baadhi ya maeneo ya Afghanistan.

Obama ameungama kwmba"Afghanistan haitokua rahisi na hii si tathimi ni yangu bali ya makamanda waliko huko."

Baadhi ya wachambuzi wanatahadharisha juu ya kuzuka hali sawa na ile iliyotokea Vietnam, katika nchi ambayo kihistoria ina uhasama na watu kutoka nje.

Rais Obama alitilia mkazo juu ya haja ya kuhakikisha kwamba magaidi wa Al Qaeda hawaishambulii Marekani na masilahi ya Marekani na washirika wake na hilo ni jambo la kwanza kupewa kipa umbele. Pia kuna haja ya kuisaidia Afghanistan kiuchumi na kuimarisha diplomasia ya Marekani nchini Pakistan.

Mahojiano hayo yamefanyika katika wakati ambao rais Obama anatarajiwa kuwasilisha pendekezo lake kuhusu Afghanistan katika mkutano wa Viongozi wa jumuiya ya kujihami ya NATO mwezi ujao, ambapo anatarajiwa kutoa wito wa msaada zaidi kutoka kwa washirika wake wa Ulaya.

Diplomasia mpya ya utawala wa Obama , mbali na Afghanistan, inatarajiwa pia kuijumuisha India kwa matumaini ya kupunguza mvutano kati ya nchi hiyo na jirani yake Pakistan, na huenda pia Iran, ambayo siku za nyuma imewapinga vikali Wataliban.

Wakosoaji kwa upande mwengine wanaonya kwamba mafanikio ya majeshi ya Marekani na Afghanistan katika kupambana na uasi nchini Afghanistan, yatategemea kwanza ni kwa umbali gani yanafanikiwa kuwaangamiza Wataliban.

Mohamed AbdulRahman/Reuters