1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria yazikosoa Mali, Niger na Burkina Faso kujitoa ECOWAS

30 Januari 2024

Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Nigeria imezikosoa tawala za kijeshi la Niger, Burkina Faso na Mali kwa uamuzi wao wa kujitoa kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS.

https://p.dw.com/p/4bq7J
Abuja, Nigeria | Rais Bola tinubu
Rais wa Nigeria Bola TinubuPicha: Temilade Adelaja/REUTERS

Kwenye taarifa yake iliyotolewa suiku wa kuamkia leo, wizara hiyo imesema uamuzi huo umeonesha mataifa hayo matatu hayana nia njema na unawanyima haki raia wao kuamua kuhusu hatma ya nchi zao. 

Nigeria iliyo mwenyekiti wa zamu wa Jumuiya ya ECOWAS imesema watawala wa kijeshi wa nchi hizo tatu ambao hawajachaguliwa na umma wameamua kuwafadhaisha raia wao kwa kuwazuia kuwa na sauti ya mwisho juu ya haki zao za kusafiri, kufanya biashara na kuwapigia kura viongozi wanaowataka. 

Soma pia:Niger, Mali na Burkina Faso zatangaza kujiondoa ECOWAS

Ukosoaji huo wa Nigeria unafuatia tangazo la siku ya Jumapili ambapo kwa pamoja Niger, Burkina Faso na Mali zilitangaza kujitoa ndani ya Jumuiya ya ECOWAS ikiwa ni mara ya kwanza kwa nchi wanachama kufanya hivyo tangu kuundwa kwa jumuiya hiyo mwaka 1975.

ECOWAS yenyeweimejizuia kutoa tamko lolote kuhusu uamuzi huo ambao utishia kuidhoofisha jumuiya hiyo ya kikanda katikati ya juhudi zake za kuzuia wimbi la mapinduzi na ukosefu usalama hasa kwenye kanda ya Sahel.