Netanyahu alikataa pendekezo la Ufaransa | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.06.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Netanyahu alikataa pendekezo la Ufaransa

Wazri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amelikataa pendekezo la Ufaransa juu ya kupitisha azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kuweka muda kwa ajili ya kuutatua mgogoro wa Mashariki ya Kati.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius akutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanjahu mjini Jerusalem

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius akutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius amelizungumzia pendekezo hilo katika ziara yake ya Mashariki ya Kati. Waziri Fabius amesema katika ziara yake ya siku mbili katika Mashariki ya Kati kwamba anayo matumaini kuwa mazungumzo baina ya Israel na Wapalestina yanaweza kuanzishwa tena.

Kwenye mkutano wake na Rais wa Israel Reuven Rivlin ,Waziri wa Ufaransa Fabius alisisitiza kwamba hakuna anaeweza kuleta mbadala wa upande wowote katika mazungumzo baina ya Israel na Wapalestina.

Waziri Fabius ameusisitiza umuhimu wa kuutatua mgogoro wa Mashariki ya Kati kwa kusema kwamba Suala la Israel na Wapalestina ni la muhimu sana. Ameeleza kuwa suala hilo pia ni muhimu kwa amani na usalama wa eneo lote la Mashariki ya Kati. Amesema kwa sababu suala hilo halijatatuliwa, linasababisha mvutano mkubwa na kwa hivyo pana hatari kubwa ya mambo kuripuka wakati wowote

Netanyahu apinga azimio

Waziri Fabius amesema Ufaransa inataka kusaidia, hata ikiwa ni vigumu kulipata suluhisho. Hata hivyo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amelikataa pendekezo la Ufaransa juu ya kupitisha azimio la Baraza la Usalama litakaloweka msingi wa kuweka muda wa kuutatua mgogoro wa Mashariki ya Kati. Netanyahu ameliita azimio hilo kuwa ni udikteta wa kimataifa.

Netanyahu alimwambia Waziri Fabius mjini Jerusalem kwamba amani itapatikana katika Mashariki ya Kati kutokana na mazungumzo ya moja kwa moja baina ya pande zinazohusika.

Licha ya kauli aliyoitoa kabla ya uchaguzi,wa nchini Israel, kuashria kwamba haliungi mkono suluhisho la kuundwa nchi mbili, Netanyahu amesisitiza kwamba anaendelea kuliunga mkono pendekezo la kuundwa nchi ya Wapalestina, lakini isiyokuwa na jeshi.

Waziri Mkuu wa Israel pia ametoa mwito kwa Wapalestina wa kurejea kwenye meza ya mazungumzo bila ya masharti yoyote. Wapalestina wanaitaka Israel iachane na mpango wa kuendelea na ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius ameikosoa Israel juu ya mpango huo. Amesema ikiwa mpango wa ujenzi wa makao ya walowezi wa kiyahudi utaendelea, juhudi za kuutatua mgogoro wa Mashariki ya Kati zitapata pigo. Hata hivyo bwana Fabius amesema usalama wa Israel lazima uhakikishwe.Lakini pia amesema kwamba haki za Wapalestina hazina budi zitambuliwe.

Mwandishi: Abdu Mtullya/afpe,dpae

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com