1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoMarekani

Nderemo zatawala utoaji wa Tuzo za Oscars

Lilian Mtono
13 Machi 2023

Kumesikika nderemo na vifijo katika ukumbi mmoja huko Kuala Lumpur, Indonesia baada ya mwanamama Michelle Yeoh kutangazwa mshindi alioupata kupitia filamu ya "Everything Everywhere All at Once".

https://p.dw.com/p/4Oc2S
95th Academy Awards | Beste Hauptdarstellerin | Everything Everywhere All at Once | Michelle Yeoh
Picha: Carlos Barria/REUTERS

Familia na jamaa za mwigizaji wa sinema raia wa Malaysia Michelle Yeoh wamekijuta wakibubujikwa na machozi ya furaha siku ya Jumatatu baada ya mwanamama huyo kutunukiwa tuzo ya Oscar ya kipengele cha mwigizaji kinara mwanamke katika filamu ya "Everything Everywhere All at Once". Tuzo hii ni ya kwanza kuchukuliwa na mwanamke raia wa Asia.

Baada ya taasisi ya Academy Awards kutangaza ushindi wa mwanamama huyo, nderemo, vifijo na hoihoi vililipuka katika ukumbi ulioko mji mkuu wa Malaysia, Kuala Lumpur ambako watu walikusanyika kufuatilia utoaji wa tuzo hizo, na macho yote yakimwelekea mama yake Michelle, Janeth Yeoh aliyekuwepo ukumbini hapo kushuhudia utoaji wa tuzo hizo.

"Ni mtu anayejishughulisha kwa bidii sana. Kila mtu anajua hilo," Janeth Yeoh, aliuambia mkutano wa waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa hafla hiyo, huku akiwa amesimama mbele ya bango kubwa lenye picha ya bintiye, Michelle iliyoandikwa "Fahari ya Malaysia."

95th Academy Awards | Bester Film | Everything Everywhere All at Once
Washiriki wa filamu ya "Everything Everywhere All at Once" wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa utoaji wa tuzo za Oscars kwenye ukumbi wa Dolby, mjini Losi Angeles.Picha: Chris Pizzello/Invision/AP/picture alliance

Nduguye Michelle, Vicki Yeoh pia aliupokea ushindi huo kwa bashasha kubwa baada ya tangazo hilo na kutiririkwa na machozi ya furaha. "Huu ni wakati wa furaha sana.... sikuweza kusema chochote, nililia, ilitokea kwa ghafla sana na tulifurahi kwamba alishinda, kwamba shangazi yetu alishinda," alisema.

Yeoh, 60, ameshinda tuzo hiyo baada ya kumuigiza mwanamke mmoja raia wa China na Marekani aliyekuwa akifanya biashara ya kufua nguo Evelyn Wang, ambaye pia alikuwa akikabiliwa na changamoto za kifamilia, katika filamu hiyo ya "Everything Everywhere All at Once", yenye maudhui ya kung fu na ucheshi.

Hii imekuwa ni tuzo ya kwanza ya Oscar kwa Yeoh na kwa kiasi kikubwa alipigiwa upatu kushinda.

Mafanikio ya mwanamama huyo huko Hollywood yalianza kuonekana alipoigiza giza kwenye filamu ya "Tomorrow Never Dies" mnamo mwaka 1997, akishirikiana na Pierce Brosnan (007). Ameigiza pia filamu ya "Coucing Tiger Hidden Dragon", Memoirs of Geisha ya mwaka 2005 na Crazy Rich Asians, 2018.

Waziri mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim amemsifu Michelle kwa mafanikio hayo akisema kazi yake imekuwa ya mafanikio makubwa na inayoendelea kuwavutia raia wengi wa Asia.